
Wamefikia hatua hiyo baada ya kutofikia muafaka katika kikao
kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam kati yao na maofisa kutoka
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra), Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, na Jeshi la Polisi Kikosi cha
Usalama Barabarani.
Akitangaza azimio hilo kwa niaba ya wajumbe waliohudhuria mkutano
huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi hayo (Taboa), Enea
Mrutu, alisema wataandika barua kuomba kukutana na Rais Magufuli ili
kumweleza matatizo yanayowasibu.
“Tukimaliza kikao hapa na kwa kuwa wote mmekubali na mnataka kukutana
na Rais Magufuli, sekretarieti itakutana tutaandika hiyo barua na
tutaipeleka nyumba nyeupe (Ikulu),” alisema Mrutu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taboa , Mohammed Hood, alisema kabla ya
kuandikia barua ya kuomba kukutana na Rais, watafanya utaratibu wa
kuonana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa.
“Hatuwezi kufika kwa Rais moja kwa moja bila kupitia kwa Waziri,
hivyo mimi nitampigia Waziri ili nimwombe tuonane na baada ya hapo
ndipo tutakwenda Ikulu,” alisema Hood.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Johansen
Kahatano, alisema hakuna uadui kati ya Sumatra na wamiliki wa mabasi na
kwamba suala la faini inayotozwa kuanzia Sh. 250,000 hadi 500,000
haliwezi kuingiliwa kwa sasa kwa sababu ni la kisheria.
“Jambo hili litafutiwe namna nyingine ya kuzungumza kwa sababu lipo
kisheria. Hakuna mmiliki atakayeshitakiwa au kupelekwa mahakamani kwa
kosa la gari kwenda kasi, dereva ndiye atakayeshitakiwa,” alisema
Kahatano.
Kahatano aliwataka Taboa kwenda Tume ya Ushindani kulalamika endapo wanaona kanuni au sheria hizo mpya zinawakandamiza.
Kuhusu kuzuia gari kwa kosa la dereva, Kahatano alisema sheria ya
Sumatra inasema endapo gari litakamatwa, mmiliki wa gari atapewa siku 14
za kulipa faini hiyo na endapo siku hizo zikipita bila kulipa, mmiliki
anaweza kufika Polisi au Sumatra na kutaka kesi iende mahakamani.
Alisema hakuna gari lolote litakalozuiwa kwa kosa alilofanya dereva na kwamba makosa ya dereva na mmiliki yametenganishwa.
Wakichangia katika mkutano huo, wajumbe wa Taboa wengi wao
walilamikia kanuni zilizokuwapo katika leseni za usafirishaji kuwa
zinawakandamiza, huku wakipendekeza faini za viwango vipitiwe upya
pamoja na makosa ya dereva na mmiliki yatenganishwe.
chanzo: zanzibar24.
Comments