Wairaki wakasirishwa na mtazamo wa kikoloni wa Marekani kwa nchi yao.

Wairaki wakasirishwa na mtazamo wa kikoloni wa Marekani kwa nchi yaoWairaki wanaendelea kubainisha hasira zao kufuatia jinai iliyotekelezwa jana na jeshi la Marekani nchini humo. Katika tukio la Jumamosi asubuhi, helikopta ya Jeshi la Marekani ilivamia eneo la Al Baghdadi katika mkoa wa Al Anbar magharibi mwa Iraq na kuua watu 8 na kuwajeruhi wengine 11.

Kufuatia jinai hiyo, Katibu Mkuu wa Harakati ya Aswaib Ahl al-Haq Bw. Qais al-Khazali ametoa taarifa na kusema: "Kufuatia hatua ya helikopta ya Marekani kudondosha mabomu katika eneo la al Baghdadi na kuuawa Wairaqi kadhaa, haikubaliki tena kuendelea kubakia Jeshi la Marekani nchini Iraq baada ya kushindwa kijeshi kundi la ISIS (Daesh).

Naye Ferdows  al-Awadi, kutoka 'Muungano wa Utawala wa Sheria' Iraq ambao unaongozwa na Nouri Al Maliki makamu wa rais wa Iraq, pia ametoa tamko na kusema: "Mapatano baina ya Baghdad na Washington ambapo yalitaka wanajeshi wa Marekani waondoke Iraq mwaka 2011 yana faida gani katika hali ambayo bado kuna vituo vya kijeshi vya Marekani katika maeneo yote ya Iraq na inaonekana kuwa vituo hivyo si vya muda.

Askari wa muungano wa Marekani unaodaiwa kupambana na ISIS wana vituo kadhaa vya kijeshi nchini Iraq kwa ajili ya kile wanachodai kuwa eti ni vita dhidi ya ugaidi.

Hii ni katika hali ambayo oparesheni za kijeshi nchini Iraq zimepelekea kuuawa mamia ya raia wasio na hatia. Aidha wanajeshi wa Iraq wamepoteza maisha katika hujuma za wanajeshi wa Marekani. 

Utendaji kazi huo mbovu wa wanajeshi wa Marekani ni dalili ya wazi kuwa wanajeshi hao vamizi hawatoi msaada wowote wenye maana katika kutatua matatizo ya  kiusalama ya Iraq. 

Matukio ya Iraq na mauaji ya kiholelea yanayotekelezwa na wanajeshi wa Marekani ni ishara kuwa, Marekani inataka kuchukua nafasi ya serikali ya kivuli katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Wanajeshi wa Marekani wamewashambulia na kuwaua  wananchi wa Iraq baada ya magaidi wa ISIS kushindwa na kufurushwa kutoka Iraq na katika upande mwingine vikosi vya Iraq vimethibtisha kuwa vina uwezo kwa kusimamia usalama kikamilifu nchini humo. 

Kwa kuzingatia nukta hizo, swali linaloibuka ni hili kuwa, je wanajeshi wa Marekani wanataka nini nchini Iraq? Je, inawezekana kutetea mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na wanajeshi wa Marekani jambo ambalo limekiuka mamlaka ya kujitawala na uhuru wa Iraq?

Baadhi ya weledi wa mambo ya kisiasa wanaamini kuwa oparesheni za kijeshi za Marekani nchini Iraq zinaashiria kurejea tena mezani ule mpango wa awali wa watawala wa Marekani wa kuikoloni Iraq. 

Aidha Marekani inalenga kuibua serikali kibaraka katika nchi hiyo kubwa ya Kiarabu yenye utajiri wa mafuta. 

Baada ya kuangushwa utawala wa kiimla wa Saddam mwaka 2003, Marekani ilimteua Jenerali Jay Montgomery Garner  kuwa liwali wa serikali ya mpito ya Iraq na baada ya hapo nafasi hiyo ilichukuliwa na Paul Bremer. 

Kufuatia kuwa macho viongozi wa kidini na wananchi wa Iraq, njama hiyo ya Marekani ya kuteua watawala wa nchi hiyo ilizimwa baada ya kufanyika uchaguzi na viongozi kuchaguliwa kwa kura za wananchi.
 
Lakini  pamoja na hayo, inaonekana Wamarekani hawakupoteza matumaini na wangali wanaendeleza mbinu za kutekeleza njama hiyo. Moja ya hatua zilizochukuliwa ni kujenga ubalozi mkubwa zaidi wa Marekani duniani mjini Baghdad. 

Ubalozi wa Marekani Baghdad una ukubwa wa ekari 104  na inasemakana ukubwa wake ni sawa na wa Vatican. Ubalozi huo pia una wafanyakazi karibu 2,000 na idadi hiyo inaendelea kuongezeka na inatazamiwa kufika  17,000. 

Swali linaliubuka hapa ni hili kuwa, je, ubalozi huo mkubwa wa Marekani unafuatilia malengo gani na ni kwa nini Wamarekani hawataki serikali ya Iraq ieneze mamlaka yake ya kujitawala katika ardhi yote ya nchi hiyo?

Katika kipindi hiki cha utawala wa Donald Trump nchini Marekani, serikali kivuli inayoongozwa na wanajeshi Wamarekani inaonekana kupata nguvu Iraq.

 Kumeshuhudiwa mara kadhaa uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika vituo kadhaa vya kijeshi Iraq na hata katika idara za kisaisa nchini humo sambamba na kuvunjiwa heshima mamlaka na uhuru wa serikali ya Baghdad. 

Mfano wa wazi ni hujuma ya wanajeshi wa Marekani dhidi ya msafara wa polisi mjini Ramadi, hujuma ambayo imetekelezwa katika fremu ya kurejesha tena mpango wa George W Bush wa kuikoloni Iraq.
chanzo: parstoday.

Comments