Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM) Wilaya ya Kinondoni, Lilian Rwebangira amesema wamelikamata gari
la meya wa jiji wa Dar es Salaam kwenye ofisi za CCM Wilaya ya
Kinondoni likiwa na vijana wawili waliovaa sare za chama hicho tawala.
Rwebangira
alidai kwamba kuonekana kwa gari hilo ni njama za Chadema kutaka
kuvuruga uchaguzi wa Februari 17 na kwamba tayari wamefikisha suala hilo
katika Kituo cha Polisi Magomeni ambako dereva wake anashikiliwa pamoja
na gari hilo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo alithibitisha kukamatwa kwa
gari hilo na kusema, “Gari lilikuwa linachunguzwa tangu jana, sasa muda
mrefu umepita, sijui wamefikia wapi katika uchunguzi huo.”
Hata
hivyo, uongozi wa Chadema umekanusha kula njama dhidi ya CCM na kusema
kwamba hiyo ni mbinu za chama hicho tawala kutaka kuvuruga uchaguzi.
Meya
wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita hakupatikana mara moja
kuzungumzia tukio hilo lakini Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema
(Bavicha), Patrick Ole Sosopi alisema kwamba jana usiku baada ya kikao
cha tathmini Mwita alilalamika kwamba dereva wake haonekani.
Ole
Sosopi alidai kwamba CCM wanataka kutengeneza mazingira ya kuvuruga
uchaguzi huo kwa kisingizio kwamba Chadema ndiyo wameanzisha.
“Inawezekanaje
dereva wa Chadema akaenda CCM! Kufanya nini? Wanajaribu ku pre-empty
ili zikitokea fujo waseme ni sisi. Ninaomba jeshi la polisi wachukue
hatua, kwa sababu hali hii haikubaliki,” alisema Sosopi.
Alidai
kwamba dereva huyo alitekwa na watu wa CCM kuanzia saa tisa alasiri na
akaachiwa saa kumi na moja alfajiri baada ya kumtesa.
Akizungumzia
tukio hilo jana, mwenyekiti huyo wa UVCCM, alisema dereva huyo wa meya
alikamatwa jana saa 2:30 usiku katika ofisi za CCM Kinondoni na
alipoulizwa alitoa sababu tofautitofauti kwamba alikwenda kuegesha na
sababu nyingine kuwa alimpeleka meya Mwita kwenye mkutano maeneo ya
jirani.
“Tulipekua
simu ya dereva na kubaini mawasiliano kati yake na meya wa jiji
akimuuliza “Uko na nani hapo?”, “Mpango unakwendaje?”. Zote hizo ni
njama za wenzetu kutaka kuvuruga uchaguzi, sasa tunaliomba jeshi la
polisi lifanye kazi yake kwa haki,” alisema Rwebangira.
Alidai
kwamba vijana wawili waliokuwa kwenye gari hilo walitoroka lakini
walitambuliwa kwa jina moja moja la Godfrey na Alex na kwamba
watalisaidia jeshi la polisi kuwapata kwa sababu wanafahamika kwa vurugu
huko Kigamboni.
“Tumekuwa
tukipokea taarifa kwamba ofisi ya meya inatumika vibaya. Hatuwezi
kuacha mambo haya yakaendelea, lazima vyombo vyetu vya dola vichukue
hatua,” alisema mwenyekiti huyo.
chanzo:Mpekuzi.
Comments