Kwa miongo kadhaa sasa Waislamu wamelazimika kucheza katika uwanja wa Wamagharibi na waungaji mkono wao katika nchi za Waislamu na kukubali mapatano na mikataba isiyokuwa na maslahi kwa mataifa ya Waislamu ili wasituhumiwe na vyombo vya habari vya Magharibi kuwa ni watu wanaopenda machafuko na ukatili.
Miongoni mwa mikataba na mapatano hayo ni ule wa Oslo kati ya utawala haramu wa Israel na Wapalestina ambao sasa unapingwa na viongozi wa harakati za ukombozi wa Palestina. Sababu ya hatua hiyo ni mwenendo wa serikali ya Marekani kuhusu mazungumzo ya amani kati ya Wapalestina na Israel.
Mwenendo huo umedhihiri zaidi mbele ya macho ya walimwengu baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuamuru ubalozi wa nchi hiyo uhamishiwe katika mji wa Baitul Muqaddas, kinyume kabisa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloutambua mji huo kuwa ni ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.
Hatua hiyo imeweka wazi zaidi kwamba Washington si mpatanishi katika mazungumzo ya pande hizo mbili bali ni mtetezi na sehemu ya Wazayuni maghasibu.
Ukweli ni kwamba, katika mwaka mmoja na ushee uliopita tangu Trump ashike hatamu za kuongoza Marekani, nchi hiyo imekuwa ikijiondoa katika mikataba ya kimataifa mmoja baada ya mwingine, suala linaloonesha kuzama na kufifia satuwa na uwezo wa Washington katika uwanja wa kimataifa.
Kujiondoa katika makubaliano ya hali ya hewa ya Paris, hatari ya kusambaratika makubalianio ya Oslo yaliyotiwa saini kwa upatanishi wa Marekani na tishio la kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni sehemu ya mafaili ya rais wa nchi asiyetaka kuwa mpatanishi na badala yake kupendelea upande mmoja na kuifanya Marekani ipewe jina la United States of Zionists.
Kutokana na hali hiyo nchi na makundi yaliyokuwa yakifanya juhudi za kujikurubisha kwa Marekani na kupata uungaji mkono wa wanasiasa wa nchi hiyo sasa zinatambua kuwa si sahihi kuitumainia Washington.
Nchi na makundi hayo yameelewa kuwa, matokeo ya aina yoyote ya mkataba na makubaliano na Marekani ni kukiukwa na kutupiliwa mbali.
Kwa msingi huo na ili kuweza kulinda maslahi ya Umma, Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kujielekeza zaidi upande wa kambi ya muqawama na mapambano badala ya kujirubisha kwa Marekani.
Huu ni ujumbe na risali ya wazi kwa serikali ya Riyadh ambayo inapaswa kurejea katika Ulimwengu wa Kiislamu badala ya kukimbilia kwenye makwapa ya Marekani na Wazayuni maghasibu.
Saudi Arabia inapaswa kuelea kwamba, kujikurubisha kwa Wamagharibi na wazayuni hakuna matokeo ghairi ya hasara na majuto.
Watawala wa kizazi cha Aal Saud ambao wanadhani kwamba, watapendwa na Donald Trump kupitia njia ya kufanya uadui na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi zote za kambi ya mapambano, wanapaswa kupata ibra na mafunzo kutokana na hatima ya vibaraka wote waliokuwa na fikra kama hiyo.
Kotohudhuria Riyadh katika vikao na mikutano ya kikanda na kimataifa ya nchi za Kiislamu ni ishara ya kutengwa au kujitenga watawala wa Saudia katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kutengwa huko kumeongezeka sana hususan baada ya kufichuliwa uhusiano wa siri wa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na serikali ya Tel Aviv.
Kwa sasa ambapo hata Wapalestina waliokuwa na fikya ya kufanya mapatano na Wazayuni maghasibu wanaanza kurejea katika kambi ya mapambano ya ukombozi, inatazamiwa kuwa, Riyadh pia itabadili udiplomasia wake na kuunga mkono jitihada za mataifa ya Waislamu za kuimarisha mapambano dhidi ya utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake.
chanzo:parstoday.
Comments