Katika taarifa yao, washiriki wa mkutano wa 13 wa mabunge ya nchi wanachama wa OIC, mbali na kutoa shukurani kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuandaa mkutano huo wamelaani uamuzi wa rais wa Marekani wa kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni na kusema kuwa hatua hiyo ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa na ni uchokozi kamili dhidi ya haki za wananchi wa Palestina.
Washiriki wa mkutano huo aidha wameunga mkono kutatuliwa changamoto zinazoendelea kuwakabili wananchi wa Palestina na kusisitiza kwamba: muqawama wa aina zote utaendelea kuwa haki halali ya Wapalestina hadi pale watakapopata haki zao hususan haki ya kurudi kwenye ardhi zao na kuunda nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Baitul Muqaddas.
Taarifa ya mwishoni mwa mkutano wa 13 wa mabunge ya nchi wanachama wa OIC imeonyesha pia wasiwasi wake kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu nchini Yemen na kusisitiza juu ya ulazima wa kutafutwa ufumbuzi wa kisiasa sambamba na kurahisishwa na kuharakishwa upelekaji misaada ya kibinadamu kwenye maeneo yote ya nchi hiyo.
Washiriki wa mkutano huo vilevile wamelaani ukiukaji wa kutisha na wa kila aina wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Myanmar katika jimbo la Rakhine na wameitaka serikali hiyo kuheshimu kikamilifu haki za kiutu na kudhamini uhuru wa msingi kwa raia wote bila ya kuwabagua kwa sababu ya asili na dini zao.
Taarifa ya mwishoni mwa mkutano huo aidha imezitaka nchi wanachama wa umoja wa mabunge ya OIC kuanzisha mfumo mpya wa kiuchumi kwa msingi wa mshikamano wa Kiislamu na kuandaa fursa na mazingira ya kustawishwa uhusiano wa kiuchumi, kimasoko, kifedha na kibenki baina ya nchi wanachama.
Mkutano wa 14 wa mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) utafanyika nchini Morocco.
chanzo:parstoday.
Comments