Sudan yaishitaki Misri UNSC kuhusiana na eneo la Hala'ib, mzozo watokota.

Sudan yaishitaki Misri UNSC kuhusiana na eneo la Hala'ib, mzozo watokotaSerikali ya Sudan kwa mara nyingine imewasilisha mashitaka yake dhidi ya Misri katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya Cairo kudhibiti eneo la Hala'ib linalozozaniwa.

Jumatatu ya jana Omer Dahab, mwakilishi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, aliwasilisha mashitaka ya nchi yake kwa Kairat Umarov, Mwenyekiti wa kiduru wa Baraza la Usalama la umoja huo. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Dahab amelitaka baraza hilo kushughulikia mashitaka hayo kama uthibitisho wa nchi yake kulalamikia hatua ya Cairo juu ya eneo la Hala'ib.
Alkhamisi iliyopita na bila kutaja sababu, serikali ya Khartoum ilimrejesha nyumbani balozi wake Abdel-Mahmoud Abdel Halim kutoka Cairo kwa kile ilichosema ni kufanya naye mashauriano ingawa hadi sasa bado hajarejea tena nchini Misri. 

Inafaa kuashiria kuwa, eneo la mpakani la Hala'ib lililopo ukingo wa Bahari Nyekundu limekuwa likizozaniwa kwa muda mrefu kati ya Sudan na Misri. 

Tangu Sudan ilipopata uhuru mwaka 1955 imekuwa ikizozana na jirani yake Misri juu ya umiliki wa maeneo ya Hala'ib na Shalateen. 
Baadhi ya duru zinaamini kuwa, safari ya hivi karibuni ya Rais Recep Tayyip Erdogan nchini Sudan imeshadidisha vita vya maneno baina ya viongozi wa Khartoum na Cairo.
chanzo: parstoday.

Comments