Qatar: Mzingiro wa Saudia, waitifaki wake dhidi yetu ni vita vya kiuchumi.

Qatar: Mzingiro wa Saudia, waitifaki wake dhidi yetu ni vita vya kiuchumiQatar imesema kukatwa uhusiano wa kidiplomasia, mzingiro na vikwazo ilivyowekewa na Saudi Arabia na waitifaki wake ni vita vya kiuchumi na Doha ipo mbioni kuhakikisha kuwa inafidiwa kutokana na hatua hizo za kiuhasama.

Katika kikao na waandishi wa habari mjini Doha jana Jumatano, Lulwah al-Khater, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar alisema tayari Doha imewasilisha lalama zake mbele ya mahakama za kimataifa na taasisi za Umoja wa Mataifa ili kushinikiza kuhitimishwa mzingiro huo.
Amesema machaguo yote yako mezani kwa Qatar na kwamba maafisa wa nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi wanafanya mawasiliano na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, juu ya kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya Saudia na waitifaki wake kutokana na mzingiro huo. 
Saudia kwa kushirikiana na nchi tatu za Kiarabu, yaani Imarati, Bahrain na Misri zilikata uhusiano wa kidiplomasia na Qatar mwezi Juni mwaka uliopita kwa madai kuwa serikali ya Doha inaunga mkono ugaidi, hatua ambayo ilienda sambamba na kuiwekea mzingiro wa kila upande nchi hiyo ya Kiarabu.
Qatar imeapa kutotekeleza orodha ya masharti 13 ya nchi hizo za Kiarabu, kukiwemo kufunga kanali ya televisheni ya al-Jazeera, kukata uhusiano na Iran na kufunga kituo cha kijeshi cha Uturuki kilichoko nchini humo ili kuondolewa vikwazo hivyo vya kidhalimu.
chanzo:parstoday

Comments