Hata hivyo bahati mbaya kwa Majimaji ni kwamba wanakwenda kucheza na Simba ambayo itakuwa chini ya Kocha mpya, Mfaransa Pierre Lechantre.
Katika mechi tatu zilizopita kwa timu hizo zilizochezwa Dar es Salaam, Majimaji haijawahi kushinda zaidi ya kupewa vipigo vikali, lakini benchi la ufundi la timu hizo imedai hizo ni zilipendwa na sasa wametua kivingine hivyo, Simba wakijidanganya wameumia.
Simba iliifunga Majimaji mabao 4-1 mwaka 2011, kisha 6-1 mwaka 2015 kabla ya kufungwa 4-0 mwaka 2016 kwenye Uwanja huo wa Taifa. Lakini, safari hii imetua wakati Lechantre akiwa kwenye benchi kwa mara ya kwanza tangu alipopewa mikoba ya kukinoa kikosi hicho cha Msimbazi chenye rekodi ya kutopoteza mchezo.
Rekodi tamu dhidi ya Majimaji zinawapa mashabiki wa Simba kila sababu ya kujazana kwa wingi uwanjani kwani, wana uhakika na ushindi. Hata hivyo, shauku kubwa ya Simba ni kutaka kuona mbinu mpya za Lechantre, ambaye ni miongoni mwa makocha wenye uzoefu na soka la Afrika.
Pia, jeuri ya Simba ipo kwa safu yake ya ushambuliaji ambayo iko moto msimu huu ikiwa imeshafumania nyavu mara 31 katika michezo 14 huku Emmanuel Okwi akiwa kinara wa ufungaji.
Simba pia imeshinda mechi tatu mfululizo za mwisho bila wavu wake kuguswa, ikiifunga Ndanda 2-0, kisha Singida United mabao 4-0 na baadaye Kagera Sugar 2-0, hivyo Mfaransa atatakiwa kukaza msuli kwelikweli.
Kocha Msaidizi, Masudi Djuma aliuelezea mchezo huo kuwa muhimu ili kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo.
“Tumejiandaa vizuri ili kuendeleza rekodi ya ushindi, tunajua Majimaji hawatakubali kupoteza kirahisi, lakini tunahitaji pointi tatu,” alisema. Hata hivyo, Majimaji licha ya kuwepo nafasi mbaya katika msimamo wa ligi, imekuwa mwiba kwa timu kubwa ikilazimisha sare dhidi ya Azam na Yanga ambazo ni wapinzani wa Simba katika mbio za ubingwa. Wakati Simba wakijivunia Okwi, mikoba ya Majimaji bila shaka itakuwa kwa Marcel Boniventure, ambaye ndiye roho ya timu hiyo akiifungia mabao matano.
“Tumekuja kucheza na malengo yetu ni kuchukua pointi tatu kwa sababu hatuko eneo zuri na ili tuepukane na hilo ni lazima tuwafunge.
Kocha wa Majimaji, Habib Kondo alisisitiza kuwa, wamekuja Dar kusaka ushindi na kuivunja rekodi mbaya dhidi ya Simba.
“Simba ni timu kubwa, ila jambo la msingi kwa vijana wangu ni kutofanya makosa,” alisema.
Comments