NEC yaeleza mzozo mpya na Mahakama uchaguzi Longido.





Ramadhani Kailima
Wakati Tume ya Uchaguzi (NEC) ikizungumzia sheria iliyotumika kuitisha uchaguzi mdogo wa Jimbo la Longido licha ya kesi iliyokuwa mahakamani kutokamilika, aliyekuwa mbunge (Chadema),  Onesmo Ole Nangole amesema wanasubiri matokeo ya rufaa yao inayoanza kusikilizwa Februari 5 kupinga kuvuliwa ubunge.
Baada ya kutangaza jimbo hilo kuwa wazi, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliilaumu NEC kwa hatua hiyo akisema rufaa ya kupinga hukumu iliyomvua Ole Nagole ubunge, ilikuwa bado mahakamani, lakini uchaguzi ukafanyika.
Jana, mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima alisema walifanya uchaguzi huo wa jimbo hilo kwa mujibu wa kifungu cha 113 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Kifungu hicho kinaeleza kuwa Mahakama, baada ya kukamilika kwa shauri au rufaa ya pingamizi la uchaguzi, itatamka kama mbunge aliyeshinda au uchaguzi unaolalamikiwa, au mtu yeyote au mtu ambaye aliteuliwa au kuchaguliwa au kwamba uchaguzi haukuwa halali na itatoa uthibitisho kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Pia kinaeleza kuwa baada ya uthibitisho, uchaguzi huo utahalalishwa au uchaguzi mdogo utaitishwa kama ambavyo kesi itahitaji kulingana na uthibitisho.
Hata hivyo wakati Kailima akisema kuwa walifanya uchaguzi kwa mujibu wa kifungu hicho, Mahakama ya Rufani inatarajia kutoa uamuzi wa maombi ya kuongezewa muda wa kukata rufaa Februari 5.
Mawakili wa Nangole, John Materu na Dancan Oola walisema wamepokea taarifa ya kuitwa Mahakama ya Rufani Februari 5 ili kusikiliza maombi yao. Materu, ambaye alipeleka maombi hayo Mahakama ya Rufaa baada ya Mahakama Kuu kutupa shauri hilo kutokana na makosa ya kiufundi, alisema wanashangazwa uchaguzi kufanyika wakati kesi inaendelea.
Kwa upande wake, Wakili Oola alisema mara baada ya Mahakama Kuu kutupa maombi ya Nangole, walikata rufaa, lakini walishangaa baadaye kuona uchaguzi unafanyika.
Alisema baada ya Tume kutangaza jimbo lipo wazi, wao waliandika barua kuijulisha kuwa bado kuna kesi inaendelea.
“Tume walinijibu wao wametangaza uchaguzi kutokana na kupata hati ya kutenguliwa ubunge kutoka Mahakama Kuu,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa kuitwa Mahakama ya Rufani kusikilizwa shauri lao, kunaibuka utata juu ya uchaguzi uliofanyika na hawajui hatma ya kesi.
Akilizungumzia suala hilo, Mbowe alisema waliiandikia Tume barua mapema ya kuitaka isiitishe uchaguzi wa Longido kwa sababu halipo wazi.
Alisema walishangaa hata walipoona NEC  imemuandikia barua Spika wa Bunge kumueleza kuwa jimbo hilo lipo wazi.
“Tukisema hatuna imani na Tume, tunaonekana wakorofi. Hivi ni mtu gani mwenye akili timamu ambaye hataona kama kuna jambo hili haliko sawa,” alisema Mbowe.
“Inakuwaje kuna kesi Mahakama ya Rufani inaendelea na haijatolewa uamuzi, jimbo linatangazwa kuwa lipo wazi. Hata baada ya kuwaumbusha kuwa jimbo hilo lina kesi na halipo wazi, hawakujali waliendelea na ratiba zao.”
Alisema imekuwa kawaida Tume hiyo kufanya kazi kwa maelekezo badala ya kusimamia misingi yake, jambo linalosababisha mgongano wa kiutendaji. “Hata sijui Nangole akishinda rufaa yake atakwenda kukaa kwenye kiti kipi, ilihali tayari uchaguzi umefanyika bila kufuata sheria.
“Nini hiki, kama siyo udhalilishaji? Kesi ya rufaa ipo na ndiyo maana mahakama imepanga siku ya kuisikiliza. Kilichofanywa na tume ni udhalilishaji,” alisema Mbowe.
chanzo:Mwananchi.

Comments