
JESHI la Polisi Mkoa wa
Kusini Pemba limesema, kuna ongezeko la kesi 47 za udhalilishaji kwa wanawake
na watoto mwaka 2017, kutoka kesi 75 ya mwaka 2016, kutokana na vitendo hivyo
kushamiri katika jamii, huku wazazi wakiendelea kuvifumbia macho pamoja na
mahakimu kwenda likizo kila mara.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake Chake
Chake, Kambanda wa Polisi Mkoa huo Sheikhan Mohamed Sheikhan alisema, mwaka
2016 walipokea kesi za udhalilishaji 75, mbapo mwaka jana walipokea kesi 122.
Alisema kuwa, mwaka jana kesi ziliongezeka 47 sawa na
asilimia 38.52, kutoka 75 ya mwaka 2016 kutokana na baadhi ya wazazi kufumbia
macho vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku kesi zikiendelea kuzorota
mahakamani kutokana na mara nyingi kwenda
likizo.
“Vitendo vya udhalilishaji vimeshamiri katika jamii, jambo
ambalo linasababisha kila kukicha kuripotiwa matukio hayo, ingawa wazazi bado wamevifumbia
macho na kuona ni jambo la kawaida”, alisema Kambanda huyo.
Kamada alieleza kuwa, kati ya kesi zilizoripotiwa mwaka 2017,
kubaka zilikuwa 33, kutorosha 45, shambulio la aibu 22, kulawiti sita (6)
ujauzito 12, kubaka kwa kikundi tatu (3) na kunajisi moja (1).
“Kati ya kesi hizo 21 zilifungwa kituo cha Polisi, 37
zilipelekwa mahakamani, kesi 55 ziko kwenye upelelezi na kesi tisa (9) zilipata
hatia”, alifafanua Kamanda huyo.
Akizungumzia changamoto ya kesi hizo, alisema ni kuwa
asilimia kubwa ya mahakimu hwenda likizo nje ya kisiwa cha Pemba, jambo ambalo
linazorotesha kesi hizo na kuchukua muda mrefu bila ya kumalizika.
“Kwa kweli utendaji umekuwa mbovu, kila siku mahakimu
wanasafiri kwenda likizo, jambo ambalo linazorotesha kesi hizi na kupelekea
Jeshi la Polisi kutupiwa lawama na wanajamii, hivyo ipo haja kwa kesi hizi
kupewa kipao mbele, ili tumalize ukatili huu unaoongezeka kwa kasi”, alisema.
Alisema kuwa, mikakati yao kwa mwaka huu watahakikisha
vitendo vya udhalilisha kwa wanawake na watoto vinaondoka kwa kuwakamata
watuhumiwa na kuwapeleka mahakamani na kuwataka watendaji wakubwa wanaokimbiza
watuhumiwa waache tabia hiyo, kwani bila ya hivyo vitendo hivyo havitoondoka.
“Tukisema tunaweka ujamaa kwenye vitendo kama hivi vya
udhalilishaji, basi itakuwa tunafanya kazi bure, hivyo kila anaepatikana na
kosa apelekwe mahakamani na endapo atapatikna na hatia ahakumiwe kwa mujibu wa
sheria”, alisema.
Aidha alieleza kuwa, kitengo cha dawati Mkoa huo kimekuwa
kikitoa elimu na mbinu za kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa
wanajamii, kutoa ushari nasaha kwa wazazi na waathiriwa na kuimarishwa huduma
bora kwa wateja wao, ili kuona kwamba vitendo hivyo vinaondoka ndani ya jamii.
“Pia mafunzo ya haki za binadamu, udhalilishaji na sheria
kinzani kwa watoto zilitolewa kwa watendaji wa dawati pamoja na Jeshi hili
kutoa misaada ya kiutu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na
hatarishi, hii ni kutokana na kuona kuwa upo umuhimu mkubwa wa kupiga vita
vitendo hivyo”, alisema Kamanda.
Kesi za udhalilishaji
kwa wanawake na watoto zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku, hivyo ni vyema
jamii, vyombo vya sheria na wadau mbali mbali kusimama, ili kuona kwamba makosa
hayo yanapata hatia ipasavyo.
Comments