Nyomi la mashabiki waliofurika Uwanja wa Chuo cha Bandari, Temeke walikuwa kila mara wakimshangilia kocha huyo kwa namna alivyokuwa akionyesha ujuzi wake kwa vitendo mbele ya wachezaji.
Ni kama vile kocha huyo ameurudisha mzuka wa mashabiki wa Simba wa kuhudhuria mazoezi ya timu yao baada ya kipindi kirefu kuuchuna kutokana na timu yao kuwanyima raha kwa kukaa miaka mitano bila taji la Ligi kuu.
Katika mazoezi hayo awali viongozi wa Simba waligoma kuwafungulia mashabiki hao, walioamua kupiga kelele kwamba wangezama ndani na geti kabla ya kuruhusiwa na kuonyesha kuwaunga mkono vijana wao na makocha uwanjani hapo.
Jambo la kushangiliwa kila mara lilimfanya kocha huyo ageuke na kuwashangaa, huku akitabasamu kwa mbali, lakini katika shangwe hizo walisikika wakimtaja kiungo Jonas Mkude wakimwambia wanamwamini na apige kazi asiwaangushe.
Mashabiki hao pia walifurahia kuwaona mastaa wao ambapo walianza kuona hata mechi iliopo mbele yao na Majimaji ya Songea watachukua pointi tatu.
SHIZA KICHUYA
Licha ya ukimya wake, lakini Shiza Kichuya kumbe naye ana vituko kwani baada ya kumaliza mazoezi yao, alipanda gari la timu na kwenda kukaa siti ya dereva na kuanza kupiga honi zilizoamsha hoihoi kwa mashabiki waliokuwa wakianza kutoka.
Kitu hicho kilikuwa burudani kwa mashabiki walimtaka Kichuya ajaribu kuliendesha hilo gari, ili waone atakavyofanya kutokana na udogo wa mwili wake.
Kichuya alijibu kuwa kazi yake ni kupiga honi ili wenzake waingie garini.
Comments