
Amesema akiwa Spika wa Bunge kuanzia Aprili 1994 hadi Desemba 2005,
chombo hicho cha dola kiliona tatizo hilo na kupitisha sheria ya
kuruhusu chaguzi ndogo kufanyika mara moja ndani ya miaka mitano, lakini
ilifutwa na Mahakama kabla ya kuanza kutumika.
“…Tuliokuwepo katika madaraka kwa muda mrefu tuliwahi kuliona
hili kwamba uchaguzi mdogo unaigharimu Serikali na walipa kodi pesa
nyingi. Kwa hiyo nikiwa Spika wa Bunge tukapitisha sheria kwamba
tusifanye uchaguzi mdogo kila unapotokea, tufanye uchaguzi mdogo mara
moja katika miaka mitano,” alisema Msekwa.
Msekwa aliyasema hayo jana baada ya kuulizwa na mwandishi wahabari
nini mtazamo wake kuhusu wanasiasa, hasa wabunge na madiwani wanaohama
vyama vyao na kusababisha chaguzi za mara kwa mara kuziba nafasi zao.
Alisema licha ya wanaohama kuwa na haki ya kufanya hivyo, chaguzi za marudio zinatumia fedha nyingi ambazo ni kodi ya wananchi.
Alibainisha kuwa sheria hiyo ilifutwa baada ya wanaharakati kufungua
kesi mahakamani na chombo hicho cha kutafsiri sheria kueleza kuwa hatua
hiyo ingewanyima haki wananchi kuwa na wawakilishi bungeni.
Katika kipindi cha mwaka mmoja kumekuwa na wimbi kubwa la wabunge na
madiwani kuvihama vyama vyao, huku madiwani sita wa Chadema katika jimbo
la Arumeru waliojiunga na CCM wakifungua dimba. Mpaka sasa Chadema
kimepoteza madiwani zaidi ya 17 na mbunge mmoja ambao wote wamehamia
CCM.
Aliyekuwa mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia naye alihamia CCM
huku aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu
akihamia Chadema.
chanzo: zanzibar24.
Comments