
Mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu mbalimbali
zikiwemo barabara na madaraja pia kubomoka kwa nyumba 377 za makazi ya
watu katika maeneo ya vijiji hivyo na nyingine 2,266 kuzingirwa na maji
hayo.
Katika taarifa ya Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Kilosa iliyosomwa
juzi na Katibu wa Kamati hiyo, Simfrosa Mollel kwa Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe, Mollel alisema takwimu hizo ni za
kuanzia tangu kutokea kwa athari za mafuriko hayo Januari 8 hadi 12,
mwaka huu.
Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua zilizonyesha katika baadhi ya
maeneo ya Kilosa na mikoa ya jirani, ikiwamo Dodoma na Manyara na
kusababisha maji kujaa Mto Mkondoa, kubomoa sehemu ya kingo ya tuta na
kuingia katika makazi ya watu na mashamba.
Alizitaja kata hizo zenye vijiji 16 kuwa ni pamoja na Mkwatani,
Chanzuri, Berega, Kidete, Magomeni, Masanze, Mbumi, Tindiga, Mbigiri na
Mabwerebwere. Mjumbe wa Kamati hiyo, Meja Yenu Mgugule alimfahamisha Dk
Kebwe kuwa, licha ya athari hizo, pia nyumba 63 zimeezuliwa mapaa
kutokana na upepo mkali uliotokea katika vitongoji vya Vikwalaza na
Tambuka Reli vilivyopo Kata ya Mikumi.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Dk Halima Mangiri alisema hatua
zilizochukuliwa ni pamoja na usambazaji wa pakiti za dawa ya kutibu maji
aina ya “waterguard” zipatazo 15,810 zilizogawiwa katika kata
zilizokumbwa na athari hizo ili kutibu maji na hadi sasa hawajapata
taarifa yoyote kuhusu kutokea kwa magonjwa ya mlipuko licha ya visima
zaidi ya 13 vya maji ya kunywa kuathiriwa na vingine kubomoka.
chanzo: zanzibar24.
Comments