Mabadiliko katika stratejia ya serikali ya uokozi wa kitaifa Yemen; kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Saudi Arabia.
Moein Shuraim aliteuliwa katika wadhifa huo Disemba mwaka 2017 na
ni mwanasiasa wa Palestina ambaye kabla ya wadhifa huo alikuwa mkuu wa
kitengo cha kisaisa cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya. Shuraim
aliwasili Sanaa, mji mkuu wa Yemen mnamo Januari 6 kwa lengo la
kufuatilia mchakato wa amani Yemen ambapo amefanya mazungumzo na
viongozi wa Ansarullah.
Aidha akiwa Sanaa amefanya mazungumzo na Bin Habtour Waziri Mku wa
Serikali ya Uokozi wa Kitaifa ambaye aliwasilisha pendekezo jipya la
kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na Saudi Arabia badala ya Abdu
Rabuh Mansour Hadi rais aliyetoroka Yemen na kukimbilia uhamishoni
Riyadh.
Swali linalojitokeza hapa ni hili kuwa, je, ni kwa nini Serikali ya
Uokozi wa Kitaifa ya Yemen imetaka kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na
Saudia?.
Jibu muhimu zaidi hapa kwa swali hili ni kuwa, viongozi wa
Ansarullah na waitifaki wake katika Serikali ya Uokozi wa Kitaifa, kwa
kudiriki uhalisia wa mambo wanataka kufikisha ujumbe huu kuwa, mhusika
mkuu katika kuibua vita na mgogoro wa Yemen si Mansour hadi bali ni
utawala wa Saudia.
Ansarullah pia imebaini kuwa hata mapinduzi yaliyofeli yaliyokuwa
yanatekelezwa na Ali Abdullah Swaleh Disemba mwaka 2017 na kupelekea
kifo chake, yalikuwa ni mtego wa Saudia kwa Swaleh katika fremu ya njama
za wakuu wa Riyadh dhidi ya Ansarullah.
Kuhusiana na hili, Hassan Hanizadeh, mtaalamu wa masuala ya kimataifa
anaamini kuwa, "uasi wa baadhi ya wafuasi wa Abdullah Swaleh dhidi ya
Ansarullah katika mji wa Sanaa, ulitokana na sera za Saudia za kuibua
mifarakano."
Sababu nyingine ya Serikali ya Uokozi wa Kitaifa ya Yemen kutaka
mazungumzo ya moja kwa moja na Saudia inatokana na kuwa, Mansour Hadi
hana uhalali wowote. Ikumbukwe kuwa kabla Saudia haijaivamia Yemen Machi
mwaka 2015, Ansarullah ilikuwa ikiamini kuwa rais wa wakati huo wa
Yemeni, Mansour Hadi, alipoteza uhalali wake baada ya kujiuzulu.
Sababu ya tatu ya Serikali ya Uokozi wa Kitaifa ya Yemen kutaka
mazungumzo ya ana kwa ana na Saudia ni kutokana na kuwa, viongozi wa
Ansarulah na waitifaki wao wana matumaini kuwa, mazungumzo ya moja kwa
moja na Wasaudia yatapunguza mgogoro wa Yemen, kwani kinyume na walivyo
Wasaudia, Ansarullah wanafungamana na usitishwaji wa mgogoro wa nchi
hiyo ambao sasa umegeuka na kuwa maafa makubwa zaidi ya kibinadamu
duniani.
Kwa msingi huo, bin Habtour katika mazungumzo yake na mwakilishi wa
mjumbe wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, viongozi wa kisiasa nchini
humo wanataka kupunguza mgogoro wa kibinadamu ambao unawakumba mamilioni
ya watu nchini humo.
Ni wazi kuwa Ansarullah na waitifaki wake
wanasikitishwa sana kuona machungu wanayoyapata raia na hivyo wanataka
kupunguza maafa hayo na ili kufikia lengo hilo wamekuwa wakiunga mkono
jitihada za amani na maelewano.
Nukta ya mwisho hapa ni kuwa, kubadilika stratijia ya mazungumzo
katika Serikali ya Uokozi wa Kitaifa ya Yemen kuna maana kuwa Ansarullah
na waitifaki wake katika serikali hiyo wanaamini kuwa, mgogoro wa Yemen
tokea mwanzo ulikuwa ni mgogoro wa Wayemen kwa Wayemen lakini baada ya
hujuma ya Saudia ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda wa miaka mitatu
sasa, mgogoro huo umebadilika na kuwa baina ya Yemen na Saudia.
Comments