LIGI ya Taifa la Soka laWanawake (Women Premier League) imepata neema baada ya kupokea udhamini mnono wa Sh 450 mil kutoka kwa kampuni ya Serengeti Breweries kupitia kinywaji chao cha Serengeti Lite ikiwa kama mdhamini rasmi wa mashindano hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa SBL Helene Weesie amesema, wameingia mkataba wa kuidhamini ligi hiyo ili kuweza kuongeza mvuto na mashabiki wa rika mbalimbali kuunga mkono, lengo iweze kufikia mafanikio makubwa kama ilivyo kwa ligi ya wanaume.
“Tunayo furaha kubwa kuwa wadhamini rasmi wa Ligi ya Taifa ya Soka la Wanawake kupitia bia yetu maarufu ya Serengeti Lite. Siku zote tumekuwa tukiamini katika kuendeleza vipaji katika sehemu mbalimbali za nchi na haswa inapokuja katika michezo inayotuleta pamoja. Tuna amini udhamini wetu utawavutia mashabiki wa rika mbalimbali kuiunga mkono ligi ya wanawake na kufikia mafanikio makubwa,” anasema Weesie.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa TFF Michael Wambura amesema, udhamini huo umekuwa ni mara ya pili baada ya kampuni hiyo awali kuwekeza katika timu yaTaifa, huku akisisitiza kampuni nyingine ziige mfano.
“Kwa mara nyingine tunashuhudia ushikiano muhimu kati yetu na SBL, kampuni maarufu ya bia na ambayo imekuwa mstari wa mbele kusaidia maendeleo ya michezo nchini. Ushirikiano huu utasaidia katika kuendeleza soka letu la wanawake pamoja na mashindano tutakayokuwa tunaandaa. Tuna furahia udhamini huu kupitia bia ya Serengeti Lite na tunaamini utakuwa wa mafanikio makubwa,”
Utiaji saini kati ya pande hizo mbili ulishuhudiwa na Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Yusuph Singo ambaye aliipongeza SBL kwa kujitolea kwake katika kuunga mkono sekta ya michezo nchini na pia kuwataka Watanzania wenye mapenzi mema pamoja na makampuni mengine kuiga mfano mzuri wa SBL.
Comments