Leo ni tarehe Mosi Januari inayosadifiana na kuanza mwaka mpya wa
2018 Miladia.
Mpangilio wa miezi ya mwaka wa Kirumi unaoanza Januari
hadi Disemba ulianza kutumiwa katika kipindi cha Mfalme Numa Pompilius
yapata miaka 700 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa Masih (as).
Kwa msingi huo
tarehe 31 Disemba huwa siku ya mwisho ya mwaka wa Miladia na usiku wa
kuamkia tarehe Mosi Januari huanza sherehe za kupokea mwaka mpya katika
jamii za Wakristo na nchi nyingi za Afrika, America, Ulaya, Australia na
hata Asia.
Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inakutakieni mwaka mpya
wenye mafanikio.
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Januari
1956, nchi ya Sudan ilipata uhuru kutoka kwa Misri na Uingereza. Mwaka
1899 Uingereza na Misri zilitiliana saini mkataba wa kuitawala kwa
pamoja Sudan.
Katikati mwa karne ya 20 lilianza vuguvugu la kutaka
kujipatia uhuru nchini Sudan na mwaka 1956 Misri na Uingereza
zikalazimika kuutambua uhuru wa nchi hiyo.
Tarehe Mosi Januari mwaka 1959 mapinduzi ya Cuba yalipata ushindi na
dikteta Fulgencio Batista akaikimbia nchi hiyo.
Ushindi wa mapinduzi
hayo yaliyoongozwa na Fidel Castro uliiweka Marekani katika mazingira
magumu baada ya kushindwa vibaraka wake nchini Cuba.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi
Januari 1993, yalianza kutekelezwa makubaliano ya Maastricht, eneo
lililoko kusini mwa Uholanzi yaliyokuwa na lengo la kuondoa mipaka ya
kiuchumi kati ya nchi 12 za Ulaya.
Mkataba wa muungano wa Ulaya ulitiwa
saini tarehe 10 Disemba mwaka 1991 na viongozi wa nchi 12 wanachama wa
Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya katika mji mashuhuri wa Maastricht.
Baadaye
Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya ilibadilishwa na kuwa Umoja wa Ulaya.
Utekelezwaji wa makubaliano ya Maastricht ulikuwa hatua kubwa katika
mchakato wa kuungana zaidi wanachama wa Umoja wa Ulaya japo kuwa umoja
huo ulikabiliwa na matatizo mengi katika miaka iliyofuatia.
Siku kama ya leo miaka 1220 iliyopita yaani tarehe 13 Rabiuthani
mwaka 218 Hijria aliaga dunia Ibn Hisham msomi na mwanazuoni mkubwa wa
Kiarabu.
Ibn Hisham alizaliwa Basra nchini Iraq na alibobea katika elimu
ya fasihi na utungaji mashairi.
Alitumia sehemu kubwa ya umri wake
kufanya uchunguzi kuhusu maisha ya Nabii Muhammad (saw).
Umashuhuri
mkubwa wa Ibn Hisham unatokana na kitabu chake cha al Sira al Nabawiyya
ambacho ni miongoni mwa marejeo muhimu kuhusu maisha ya Mtume Muhammad
(saw).
Comments