Leo ni siku ya Ijumaa tarehe 12 Januari, 2018 kama kawaida yetu tunakuletea kipengele cha kumbu kumbu.

Leo ni Ijumaa tarehe 24 Rabiuthani mwaka 1439 Hijiria inayosadifiana na tarehe 12 Januari mwaka 2018.

Miaka 39 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliagiza kuundwa Baraza la Mapinduzi katika kipindi hicho muhimu cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. 
Imam aliagiza baraza hilo liundwe wakati Marekani ilipokuwa ikifanya njama za kuulinda utawala wa kifalme wa Pahlavi. 
Jukumu kubwa la baraza hilo lilikuwa ni kuratibu mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na pia kuandaa uwanja mzuri wa kuundwa serikali ya muda nchini Iran.
شورای انقلاب
Miaka 353 iliyopita katika siku inayosadifiana na leo, aliaga dunia Pierre de Fermat mwanahisabati wa Kifaransa na mwasisi wa nadharia ya leo ya namba yaani Modern Theory of Numbers na ile ya uwelekeo inayojulikana kama Theory of Probability. 
Pierre de Fermat alizaliwa mwaka 1601 Miladia na alianza kujifunza hesabu tangu akiwa mtoto. Mwanahisabati huyo wa Kifaransa aligundua pia kanuni msingi ya jiometri changanuzi, yaani Analytic Geometry.
پیر دو فرما
Mwaka 388 Hijiria katika siku kama ya leo, alifariki dunia mtaalamu wa lugha na alimu wa Kiislamu, Abu Ali Muhammad bin Mudhaffar maarufu kwa jina la Hatami au Baghdadi. Alipata elimu kwa walimu mashuhuri wa wakati huo na baadaye alianza kufundisha masomo ya lugha mjini Baghdad. 
Shule ya Hatami haikuwa na mithili katika zama hizo na wasomi wakubwa wa zama zile walikuwa wakishiriki katika vikao vya darsa za Abu Ali Muhammad bin Mudhaffar. Miongoni mwa vitabu vya mtaalamu huyo ni pamoja na kile cha "Hatamiya" kinachokosoa mashairi ya malenga wa zama zake.
ابوعلی محمد بن مظفر
Miaka 602 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani mwaka 837 Hijiria, katika kipindi cha watawala wa Teimur alifariki dunia malenga wa Kiirani, Sayyid Qasim al Anwar. 
Alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa na mwenyeji wa mji wa Tabriz ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. 
Baada ya kuishi na kufundisha katika mji wa Harat huko kaskazini magharibi kwa Afghanistan, Sayyid Anwar alianza kupata umashuhuri, kiasi kwamba walijumuika kwake wanafunzi na wafuasi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. 
Hata hivyo kutokana na dhana mbaya ya watawala wa wakati huo dhidi ya malenga huyo, Sayyid Qasim al Anwar, alilazimika kuhama kutoka Harat kwenda Samarqand nchini Pakistan ya leo. Miongoni mwa athari za malenga huyo ni pamoja na diwani ya mashairi na vitabu vya "Anisul Arifina" na " Anisul Aashiqina." 
آرامگاه سید قاسم انوار
Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita mhadhiri wa nyuklia wa Chuo Kikuu cha Tehran, Dokta Massoud Ali-Mohammadi aliuawa kigaidi. Massoud Ali-Mohammadi aliyekuwa na umri wa miaka 50 aliuawa wakati alipokuwa akitoka nyumbani kwake kwa mlipuko wa bomu la kuongozwa kutoka mbali. Alipata shahada ya uzamivu ya taaluma ya fizikia katika Chuo Kikuu cha Shariif mjini Tehran mwaka 1371 na alikuwa miongoni mwa wanachuo wa kwanza wa Iran kupata shahada ya uzamivu ya somo la fizikia ndani ya Iran. Alitunukiwa tuzo ya Tamasha ya Kimataifa ya Kharazmi mwaka 1386 na kushika nafasi ya pili katika utafiti wa masuala ya kimsingi.
Wapinzani wa miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran baada ya kushindwa kusimamisha miradi hiyo kwa hatua za kisiasa na vikwazo vya kiuchumi walikhitari kutumia njia za kigaidi na kuwaua wasomi wa nyuklia wa Iran. Magaidi waliomuua msomi huyo wa Iran walitiwa nguvuni na kukiri kwamba walikuwa wakishirikiana na utawala haramu wa Israel.
مسعود علی محمدی
Na siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 7 kwa kipimo cha Rishta ilitokea huko Haiti katika bahari ya Caribbean. Zilzala hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea duniani katika miongo kadhaa iliyopita na iliua watu karibu laki tatu na kujeruhi wengine wengi. Mtetemeko huo wa ardhi ulioikumba Haiti uliharibu kabisa miundo mbinu na nyumba nyingi za nchi hiyo. Aidha ulipelekea mamia ya maelfu ya raia kuwa wakimbizi.
زلزله هائیتی
 kipengele hichi kimeletwa kwenu na parstoday.

Comments