MABEKI wa Simba, Mghana Asante Kwasi na Juuko Murshid raia wa Uganda, wameshindwa kuanza mazoezi ya pamoja na kocha wao mpya, Pierre Lechantre kutokana na kuwa majeruhi, lakini daktari wa kikosi hicho, Yasin Gembe amesema, watakuwa sawa mapema iwezekavyo.
Kwasi na Juuko wote wanacheza beki ya kati katika kikosi cha kwanza, lakini wamekutwa na tatizo hilo kutokana na kupata majeraha hayo kwenye mchezo wao uliopita walipoifunga Kagera mabao 2-0.
“Wachezaji hawa wana maumivu madogo tu ya kawaida, Kwasi anasumbuliwa na enka na Juuko msuli wa paja wanaendelea na matibabu na mazoezi mepesi si muda watajiunga na wenzao,” alisema Gembe.
Lechantre na msaidizi wake, Mtunisia Mohammed Aymen, wameanza kazi rasmi ya kuifundisha Simba juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Bandari jijini Dar es Salaam.
Simba ambao ni vinara wa Ligi Kuu Bara wakiongoza na pointi 32, wanajiandaa na mchezo dhidi ya Majimaji utakaochezwa wikiendi hii jijini Dar es Salaam.
Mbonde anarudi
Wakati Juuko na Kwasi hali ikiwa hivyo, beki mwingine wa kati ya timu hiyo Salim Mbonde anatarajiwa kuungana na wenzake mapema mwezi ujao baada ya kupona maumivu ya goti. Beki huyo ameanza kujifua taratibu asubuhi na jioni.
Mbonde aliumia mwanzoni mwa msimu, baada ya matibabu na mapumziko, ameanza kupambana na mazoezi.
“Nimeanza mazoezi binafsi na nafanya mara mbili kwa siku,” alisema.
Comments