Kimbunga hicho cha Ava kilichoikumba Madagascar mwishoni mwa wiki iliyopita kiliathiri zaidi maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo na kilikuwa na kasi ya kilomita 140 na 190 kwa saa.
Afisa Mawasiliano wa Ofisi ya Taifa ya Kusimamia Maafa, Venise Melisa amethibitisha kuwa kimbunga hicho kimeua watu wasiopungua 29 na kwamba 8 kati ya waliouawa walikuwa watu wa familia moja.
Ofisi ya Taifa ya Kusimamia Maafa ya Madagascar imetangaza kuwa, watu wengine 13 elfu wamepoteza makazi na nyumba zao kutokana na kimbunga hicho na kwamba shule zimefungwa hadi leo Alkhamisi kwa kuhofia mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Mwezi Machi 2017, kimbunga Enawo kiliikumba Madagascar na kuua watu wasiopungua 78 kwenye pwani yake ya kaskazini mashariki, eneo ambalo ni maarufu kwa kuzalisha zao la vanilla.
Kimbunga hicho cha Enawo kiliharibu karibu asilimia 30 ya zao la vanilla katika nchi hiyo ambayo ni mzalishaji mkubwa zaidi wa zao hilo dunia. Madagascar inazalisha karibu nusu ya zao hilo duniani.
chanzo:parstoday.
Comments