![]() |
KIKOSI
cha Simba kinaendelea kuongoza Ligi Kuu Bara baada ya ushindi wa mabao
2-0 dhidi ya Ndanda FC, mechi iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Nangwanda
Sijaona mjini Mtwara.
Ushindi
huo unakuwa ni wa saba kwa Simba dhidi ya timu hiyo ya Mtwara, lakini
ni furaha kubwa kwa Kocha Mkuu wa Muda wa Simba, Irambona Masoud Djuma
raia wa Burundi ambapo ndiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza akiwa bosi.
Djuma, kocha wa zamani wa Rayon Sports, amechukua nafasi hiyo baada ya uongozi wa Simba kuamua kuachana na Kocha Joseph Omog.
Omog
ambaye aliwahi kubeba ubingwa na Azam FC bila ya kupoteza hata mechi
moja, ameondoka akiwa ameiachia Simba historia nzuri kabisa ya
kuibebesha ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports ambalo ndilo
lililomponza baada ya kuvuliwa na Green Worriers inayoshiriki ligi
daraja la pili.
Kocha
huyo Mcameroon, ndiye aliyeirejesha Simba katika michuano ya kimataifa
baada ya ubingwa huo wa Kombe la Shirikisho lakini ndiye aliyeirudisha
Simba katika ushindani sahihi dhidi ya Yanga.
Kwa
misimu minne mfululizo, ukiwemo ule mmoja ambao Omog alibeba ubingwa
akiwa na Azam, Simba imekuwa ikishika kuanzia nafasi ya tatu hadi ya nne
na moja na mbili zilikuwa ni Yanga au Azam FC.
Msimu
wa mwisho, Omog aliipa Simba nafasi ya pili tena ikilingana pointi na
mabingwa Yanga lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa,
ikawaangusha.
Baada
ya kuondoka Omog, Simba imempa nafasi hiyo Djuma lakini bado inaonekana
ina hofu kwa kuwa Djuma anaweza asiwe na nguvu za kutosha kukiongoza
kikosi hicho katika michuano ya kimataifa.
Huenda
huko mbele lakini kwa timu za mwanzo, mfano Gendamarie ya Djibouti
ambayo Simba wamepangiwa kuanza nayo, kocha huyo hatakuwa na presha hata
kidogo.
Lakini
Simba pia hawako katika mstari mbaya kwa kuamua kuangalia kocha gani
anaweza kuwasaidia katika michuano hiyo ya kimataifa na ikiwezekana
kubeba angalau ubingwa wa Tanzania Bara wanaousubiri kwa hamu na
ikizingatiwa, hawana tena ubingwa wa Kombe la FA.
Awali
ilielezwa anaweza kubaki Djuma na Selemani Matola akarejea na kuwa
msaidizi wake. Lakini baadaye kumekuwa na majina ya makocha wengi kutoka
nje na inaonekana Simba imepania kuleta Mzungu.
Majina
mawili ndiyo yana nafasi kubwa, huenda akawa Kim Poulsen raia wa
Denmark ambaye amekuwa akizifundisha timu za vijana za Tanzania na pia
muda mfupi aliinoa Taifa Stars.
Kocha
wa pili ni Goran Kopunovic, huyu ni raia wa Serbia aliyewahi kuinoa
Simba kwa miezi kadhaa na kuiwezesha kubeba Kombe la Mapinduzi.
Makocha
wote wawili ni wazuri lakini kumekuwa na taarifa ya mvutano mkubwa kati
ya wajumbe wa kamati ya usajili kwa kuwa ni jambo la kawaida wao pia
kujadili na kutafakari kabla ya kumpata mchezaji au kocha wanayemtaka.
Kwa maana ya ubora, hakuna anayeweza kumpinga Poulsen ambaye hii ni mara ya pili, Simba inaonyesha nia ya kutaka kumpata.
Lakini
ni kocha ambaye alikuwa akizinoa timu za taifa tangu ametua nchini,
hatujawahi kuiona nguvu yake katika kikosi cha klabu. Huenda linaweza
kuwa ni chaguo zuri lakini litakuwa ni suala la kujaribu tena kwa Simba.
KOPUNOVIC |
Maana
yake itakuwa hivi; Simba inaweza kumjaribu Djuma kuona kama ataweza kwa
kuwa aliiongoza Rayon Sports ya Rwanda kucheza michuano ya kimataifa,
hivyo anaweza kuiongoza Simba.
Kumchukua
Poulsen ni kujaribu mara ya pili, kwa kuwa naye hatujawahi kuiona nguvu
yake katika ngazi ya klabu. Hivyo, Simba wataendelea kujaribu kwa
makocha wawili ndani ya wakati mmoja.
Katika
soka, suala la kujaribu lipo na wakati mwingine linakuwa ndiyo au
hapana. Hivyo wakiamua kujaribu ni suala la kukubali matokeo
yatakayofuatiwa hasa kama Poulsen atazidiwa na presha kwa kuwa ile ya
timu ya taifa inakuwa chini sana.
Kopunovic,
hata kama Simba itakuwa inajaribu, itakuwa ikifanya hivyo kwa nafasi
kubwa sana ya kujiamini kwa kuwa ilifanya kazi na kocha huyo kwa nusu
mwaka.
Anaiweza
presha ya Simba, kazi yake ilionekana ni nzuri na hata kuondoka kwake
si kwamba alishindwa kazi badala yake alipotaka kulipwa ada ya usajili
na Simba haina kitu, safari yao ikaishia hapo.
Kocha
huyo aliitoa Simba kutoka nafasi ya nane na kuirejesha kwenye ushindani
katika nafasi ya tatu, pili na kuirudisha tena kuwa na hadhi yake.
Usisahau,
ndiye kocha aliyeanza kuwapa wachezaji wengi nafasi ya kucheza tena
wale waliokuwa hawaaminiki na mmoja wao ni Said Ndemla.
Simba
inaweza kuamua chochote kati ya haya matatu, lakini lengo litakuwa ni
kujenga. Kibaya zaidi kamati inaweza kujichanganya kwa matakwa binafsi
wakati wa kujadili masuala yao kuhusiana na kupata mtendaji sahihi.
Wajumbe
wanapaswa kujadili mambo kwa maslahi ya Simba kwa lolote lile
wanalotakiwa kufanya badala ya kuanza kufikiria urafiki wao na fulani au
la.
Wakati
Kopunovic akiondoka, alikorofishana na baadhi ya viongozi wa Simba na
baadhi wako kwenye kamati, wengine hawapo. Sasa wale walio kwenye
kamati, kama wanaona kuna sababu za msingi kumkataa kocha huyo
wanatakiwa kuweka mezani zijadiliwe lakini si kufikiria uhusiano wao.
Hakuna
urafiki au uadui wa kudumu hasa unapozungumzia kazi au biashara.
Kikubwa viongozi wenye nafasi Simba wajue hiyo ni klabu ya watu na
wamepewa dhamana, wasijisahau.
Matakwa
binafsi weka kando unapofikia kujadili maslahi ya klabu kwa kuwa
kufanya hivyo ni kuonyesha kuwa Simba ni sawa na gari lako au nyumba
yako na unaweza kuamua unachotaka kufurahisha nafsi yako, hili ni jambo
baya kabisa kwa kiongozi anayejielewa.
Comments