Oktoba 13 mwaka jana, Rais Trump sambamba na kukataa kuthibitisha kufungamana Iran na makubaliano ya nyuklia alitishia kujitoa nchi yake katika makubaliano hayo na akalikabidhi suala la maamuzi kuhusiana na JCPOA kwa Kongresi ya nchi hiyo. Rex Tillerson, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Shirika la Habari la Associated Press kwamba, katika kipindi cha siku chache zijazo, Trump atayafanyia marekebisho makubaliano ya nyuklia au ataiondoa Marekani katika makubaliano hayo.
Akizungumza katika mkutano wa usalama mjini Tehran siku ya Jumatatu Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni anayehusika na masuala ya kisheria na ya kimataifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na kutoa indhari kuhusiana na hatua tarajiwa ya Rais wa Marekani ya kusambaratisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA alisema kuwa, Iran imejiandaa kikamilifu kwa ajili ya kukabiliana na senario zote kuhusiana na makubaliano hayo.
Njama za kutaka kuvuruga makubaliano ya nyuklia bila ya kuweko ushahidi wa wazi wa kuonyesha kwamba, Iran imekiuka makubaliano hayo, ni jambo ambalo linaweza kupelekea kusambaratika kundi la 5+1 linaloundwa na nchi za Marekani, Ufaransa, Russia, China, Uingereza pamoja na Ujerumani.
Kwa hakika kuvurugwa na kufutwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kutakuwa na matokeo mengine pia kwa jamii ya kimataifa. Huo utakuwa ni ujumbe wa wazi kwa walimwengu kwamba, Marekani haina uwezo wa kutekeleza makubaliano ya kimataifa kutokana na muundo wake wa kisiasa.
Bila shaka ufahamu huo utakwamisha kufikiwa makubaliano na Marekani katika masuala mengine.
Uamuzi wa Trump katika siku chache zijazo kuhusiana na kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA bila shaka una umuhimu mkubwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; kwani makubaliano hayo yaliidhinishwa na kuungwa mkono na baraza hilo kupitia azimio lake nambari 2231 na kufutwa au kufanyiwa mabadiliko ya aina yoyote ya upande mmoja kutalitilia alama ya swali azimio hilo.
Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana misimamo ya Marekani imeutia wasiwasi pia Umoja wa Ulaya.
Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya mwaka jana alifanya safari mjini Washington Marekani na kufanya juhudi za kuwakinainisha viongozi wa Marekani pamoja na Kongresi ya nchi hiyo juu ya kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Hata hivyo inaonekana kuwa, juhudi hizo hazikuwa na natija ya maana. Hii ni katika hali ambayo, akthari ya viongozi wa Marekani wanatambua kwamba, kufutilia mbali makubaliano hayo litakuwa kosa kubwa.
Wanajeshi kadhaa wastaafu, wajumbe wa Baraza la Kongresi na wanadiplomasia wakiwemo wataalamu 52 wa usalama wa taifa wa Marekani wameandika barua wakiitaka serikali ya Trump isiyahatarishe makubaliano ya nyuklia na Iran. Msemaji wa Umoja wa Ulaya ametangaza kuwa, Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa umoja huo, kesho Alkhamisi tarehe 11 Januari atakuwa mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Iran mjini Brusseles Ubelgiji.
Alaa kulli haal, uamuzi wa siku chache zijazo wa Marekani kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni mtihani wa kupima kiwango cha maamuzi ya kimataifa na asasi za kimataifa zenye itibari kama Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Hadi sasa wakala huo, umethibitisha mara tisa juu ya kufungamana kikamilifi Iran na makubaliano hayo ya nyuklia. Linalosubiriwa sasa ni kuona asasi hiyo kama ulivyo Umoja wa Ulaya na wanachama wengine wa Baraza la Usalama inaweka wazi msimamo wake kuhusiana na ukiukaji ahadi wa Marekani pamoja na ukwamishaji mambo wa Washington wenye madhara.
chanzo:parstoday.
Comments