Equatorial Guinea yasema jaribio la mapinduzi lilipangwa Ufaransa.

Equatorial Guinea yasema jaribio la mapinduzi lilipangwa UfaransaSerikali ya Equatorial Guinea imesema jaribio la mapinduzi lililofeli mwishoni mwa mwaka uliomalizika wa 2017 liliratibiwa ndani ya ardhi ya Ufaransa.

Agapito Mba Mokuy, Waziri wa Mambo ya Nje wa Equatorial Guinea amesema wana taarifa za kiintelijensia zinazothibitisha kuwa jaribio hilo la mapinduzi lilipangiwa nchini Ufaransa na kwamba watashirikiana na serikali ya Paris katika uchunguzi wakishapata taarifa zaidi.
Hata hivyo amesisitiza kuwa serikali ya Ufaransa haikuhusika kivyovyote kwenye jaribio hilo lililofanyika siku moja kabla ya Krismasi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Equatorial Guinea amebainisha kuwa, 'mamluki au magaidi' 27 wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na jaribio hilo, na kwamba maafisa usalama wanaendelea kuwasaka wengine 150 wanaodaiwa kujificha katika mpaka wa nchi hiyo na Cameroon.
Disemba 24 mwaka jana na baada ya kutibuka kwa jaribio hilo la mapinduzi dhidi ya serikali, polisi walivamia majengo ya ofisi za chama cha upinzani cha Citizens for the Innovation katika miji ya Malabo na Bata, miji mikuu ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo na kuwatia mbaroni makumi ya wafuasi wa chama hicho.  
Nchi hiyo ndogo ya Kiafrika yenye utajiri wa mafuta imekuwa ikiongozwa na Rais Teodoro Obiang Nguema tangu mwaka 1979.
CHANZO:parstoday

Comments