Katika mahojiano na shirika la habari la AFP pambizoni mwa mkutano wa
AU mjini Addis Ababa, Francisco Madeira, Mkuu wa Amisom amesema ana
wasi wasi mkubwa kwamba huenda mafanikio yote waliyoyapata katika
kipindi cha muongo mmoja uliopita yakaporomoka, iwapo wataondoa ghafla
askari wote 21 elfu wa kikosi hicho bila kuweka mikakati madhubuti ya
kukabidhi mikoba kwa maafisa usalama wa Somalia.
Amesema, "Jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuhakikisha kwamba
mchakato wa kukabidhi jukumu la usalama kwa askari wa Somalia
unafanikiwa."
Madeira amesema Amisom iliwaondoa nchini Somalia askari wake elfu
moja kufikia mwishoni mwa mwaka uliomalizika, na inatazamia kuondoa
idadi kama hiyo kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Kikosi cha Amisom ambacho kiliundwa kupitia azimio la Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa kimekuwa kikiisaidia serikali ya Somalia
kupambana na magaidi wa kundi la al Shabab tangu mwaka 2007.
Kikosi hicho kinaundwa na askari kutoka nchi za Uganda, Kenya, Djibouti, Burundi na Ethiopita.
Comments