
Dk. Shein alisema hayo leo mara baada ya ufunguzi wa barabara ya
Jendele, Cheju hadi Unguja Ukuu ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za
miaka 54 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964.
Dk. Shein alieleza kuwa vijana wa Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa
Barabara (UUB) wana utaalamu mkubwa lakini kinachowakwaza ni ukosefu wa
vifaa pekee na kueleza kuwa ujenzi unaofanywa na mafundi wazalendo
hupelekea kujenga barabara imara kwa fedha kidogo ikifananishwa na
Kampuni za kutoka nje ya Zanzibar.
Alisisitiza haja ya kujitegemea katika kujenga barabara za hapa
nchini na ndipo Serikali imeamua kutoa fedha kwa ajili ya kununua vifaa
ili kuendeleza shughuli hizo kwa ufanisi mzuri zaidi huku akisisitiza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kufanya mambo
yake.
Dk. Shein aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni mpango wa
Serikali wa kujenga barabara hiyo na wala Serikali haijakurupuka kwani
barabara hiyo itasaida katika usafirishaji wa mazao mbali mbali yakiwemo
mpunga pamoja na bidhaa nyengine na wananchi.
Alisema kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yameleta umoja na usawa
miongoni mwa wananchi wa Zanzibar na wala hayajambagua mtu kwa rangi
yake, dini yake, kabila lake na yote yanayofanywa Unguja yanafanywa na
Pemba, na yanayofanywa mjini hufanywa na vijijini.
Aidha, alieleza kuwa Serikali anayoiongoza haimbagui mtu na yote
yanayofanywa yameanza kufanywa na Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu
mzee Abeid Amani Karume na kusema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
ni Serikali ya wananchi wote wa Zanzibar.
Alieleza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo na kwa upande
wa sekta za maendeleo Zanzibar imepiga hatua kubwa ikifananishwa na
nchi nyengine za bara la Afrika.
Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara pamoja na Idara ya
Ujenzi na Utunzaji wa Barabara (UUB) kwa kazi nzuri waliyoifanya pamoja
na kufikiria haja ya kuongeza urefu wa barabara kwa urefu wa kilomita
mbili zinazojumuisha mzunguko wa makutano ya barabara ili kuweka vizuri
matumizi ya barabara hiyo.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisisitiza usemi wa wazee kuwa “Subira
huvuta heri” na “Baada ya dhiki faraja” kutokana na uvumilivu uliotokea
baada ya kushindwa kwa Kampuni ya ujenzi iliyoanza kujenga Barabara
hiyo.
Alieleza makubaliano yaliofikiwa kati ya Serikali na Benki ya
Maendeleo ya Kiarabu ya Maendeleo ya Uchumi ya Afrika (BADEA) kuwa
Serikali ikamilishe ujenzi wa barabara hiyo ya Jendele-Cheju-Kaebona kwa
kiwango cha lami kwa kutumia fedha zake za ndani na BADEA itaendelea
kuifadhili barabara ya Koani-Jumbi kwa bakaa ya fedha zilizobakia kwa
mujibu wa mkataba wa fedha baina ya Serikali na Benki ya (BADEA).
Dk. Shein alieleza madhumuni ya barabara ikiwa ni pamoja na
kusafirisha mazao pamoja na bidhaa nyengine ikiwa ni pamoja na
kuwasaidia wananchi kusafiri wao wenyewe kutoka sehemu moja kwenda
nyengine.
Alisema kuwa hivi sasa Zanzibar ina mtandao mzuri wa barabara
ikifananishwa na wakati kabla ya Mapinduzi ya Januari 1964 ambapo baada
ya hapo ndipo barabara nzuri zilipotengenezwa na kusisitiza kuwa kabla
ya Mapinduzi hayo maeneo machache tu ndio yaliokuwa na barabara za lami.
Aidha, aliwaeleza wananchi haja ya kuzitumia barabara kwa maendeleo
na kuwataka wananchi hao kuitunza na kuienzi barabara hiyo ili iweze
kudumu kwa muda mrefu huku akiwaeleza wananchi azma ya Serikali ya
kuubadilisha mji wa Zanzibar kwa kujenga majengo sambamba na miji ya
kisasa ndani yake.
Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Balozi Ali Abeid
Karume alitoa shukurani kwa juhudi zake na ahadi zake sambamba na kuipa
upendeleo Wizara yake ili iweze kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo
sambamba na kuwapa miongozo na hatimae barabara hiyo imekamilika.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa
Aboud Jumbe akitoa maelezo ya kitaalamu alisema kuwa ujenzi wa
barabara hiyo ni moja wapo ya jitihada ambazo Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imekuwa ikichukua tokea Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ya
kujenga ustawi wa wananchi wake kwa kuimarisha na kuendeleza miundombinu
ya barabara mijini na vijijini Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake
aliyoitoa tarehe 5 Aprili 2016 wakati wa uzinduzi wa Baraza za Tisa la
Wawakilishi.
Aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulianza rasmi mwezi Januari
2013 kwa lengo la kujengwa kwa barabara tatu kwa kiwango cha lami,
barabara hizo ni pamoja na Barabara ya Koani-Jumbi kilomita 6.3 na
Kizimbani-Kiboje kilomita 7.2 na ulitegemewa kuchukua muda wa miezi 17
hadi kukamilika kwakwe.
Alieleza kuwa mradi huo unafadhiliwa na Benki ya (BADEA)
ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ulitarajiwa
kugharimu TZS Bilioni 14.8 ambapo mradi huo ulianza kutekelezwa na
Kampuni ya DB Shaprya kutoka Dar-es-Salaam na kusimamiwa na Kampuni ya
Newtech Industrial Engineering Group kutoka Sudan ikishirikiana na
Kampuni ya EM Consult ltd kutoka Tanzania.
Aidha, Katibu Jumbe alieleza kuwa Kampuni ya DB Shapriya ilishindwa
kukamilisha kazi hiyo kwa wakati ambapo ilifikia asilimia 24 tu ya kazi
yote aliyokabidhiwa kwa mujibu wa muda ulioanishwa katika Mkataba wa
ujenzi wa barabara hizo licha ya kuongezewa miezi 13 aliyoomba lakini
alishindwa kukamilisha na ndipo Wizara ilipovunja nae Mkataba.
Kutokana na hali hiyo Serikali iliamua kutumia wataalamu wake kutoka
Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara (UUB) ambapo kazi hiyo
ilikamilika mwezi Julai, 2017 na kuitengeza barabara hiyo yenye kilomita
13 kwa kiwango cha lami.
Aliongeza kuwa hadi Julai 2017 jumla ya TZS Bilioni 6.1 zimetumika
katika utekelezaji wake kwa kazi za ujenzi, kati ya fedha hizo jumla ya
TZS Bilioni 3.7 ni kutoka BADEA na TZS Bilioni 2.4 ni kutoka Serikalini.
Katibu Jumbe alitoa shukurani kwa Dk. Shein ambapo Serikali
anayoiongoza imetenga jumla ya TZS Bilioni 5.5 kwa ajili ya ununuzi wa
vifaa vya Ujenzi wa barabara ikiwemo mtambo wa kupikia lami, gari la
kutandaza lami iliyopikwa na gari la lami ya maji ili kuijengea uwezo
Idara ya UUB pamoja na ununuzi wa tani 1,700 za lami kwa matumizi ya
Unguja na Pemba.
Viongozi pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali walihudhuria
katika hafla hiyo iliyokwenda sambamba na burudani iliyotolewa na
vikundi vya ngoma za utamaduni.
chanzo:Zanzibar24
Comments