WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa
Halmashauri na Maafisa Kilimo kutoka mikoa inayolima korosho,
washirikiane kupata takwimu mpya za wakulima wa zao hilo.
Ametoa
agizo hilo jana mchana (Jumapili, Desemba 31, 2017) wakati akizindua
kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 msimu
wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi.
“Maafisa
kilimo na maafisa ushirika mkisimamiwa na Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi,
mshirikiane na kusimamia kwa umakini upatikanaji wa takwimu za wakulima
na maeneo yanayolimwa, haiwezekani kila mwaka takwimu ziwe ni zilezile
tu,” alisema.
“Afisa
kilimo wa wilaya lazima ujue una wakulima wangapi, je hao wakulima
wako, kila mmoja analima ekari ngapi? Na katika ekari hizo, ana miche
mingapi, na je ana mahitaji ya pembejeo kiasi gani?” alisema.
“Pia
nilikwishawaagiza maafisa ushirika na viongozi wa vyama vya msingi
(AMCOS) mpaka chama kikuu cha ushirika, kuwa kila mmoja anapaswa atambue
ana wanachama wangapi katika chama chake. Hili litawezekana pia kwa
kushirikiana na Afisa Mtendaji wa Kata au Mwenyekiti wa Kijiji, kwa
sababu wao wana idadi kamili za watu wanaowaongoza,” alisema.
“Ninaamini
tukifanya hilo tutamaliza tatizo la takwimu na Serikali itakuwa na
uwezo mkubwa wa kuwahudumia wakulima wake, na tutaweza kuweka bajeti ya
kutosha kuhudumia mahitaji yao,” alisisitiza.
Waziri
Mkuu alipanda mche mpya wa korosho ili kuanzisha zoezi la upandaji
miche hiyo na kisha akagawa miche kwa wakulima 10 kutoka vijiji vya
Likunja, Kitandi, Kilimahewa na Nachingwea ambao waliwawakilisha wenzao.
Mapema,
kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alikagua vitalu vya miche
ya mikorosho vilivyopandwa na Halmashauri ya Ruangwa na kuelezwa kuwa
miche hiyo ipo ya aina mbili ambapo aina ya kwanza ni ile iliyotokana na
mbegu na ya pili ni ile iliyotokana na vikonyo (grafting).
Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka jimboni kwake.
Sherehe
hizo zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na
wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya na wataalamu
kutoka kituo cha utafiti cha Naliendele walishiriki zoezi hilo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 31, 2017.
Chanzo:Mpekuziblog.
Comments