Jose Mourinho wa Manchester United.
KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema Jose Mourinho wa Manchester United anatakiwa kupambana na hali yake na kuacha kulialia kuhusu gharama za usajili uliofanywa na Manchester City.
Mara baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Burnley, Mourinho alisema kiasi cha pauni milioni 300 alichotumia kusajili tangu msimu uliopita hakitoshi kupambana na Man City kwa kuwa wao wametumia zaidi ya pauni milioni 360 kusajili.
Akizungumzia sual hilo, Wenger ambaye mara kadhaa amewahi kukwaruzana na Mourinho, amesema kupambana na timu zinazotumia gharama kubwa kusajili ni jambo la kawaida kwake na hata Mourinho anatakiwa kuzoea.
Arsene Wenger
“Nimekuwa katika hali hiyo kwa miaka 21, siwezi kuanza kulalamika sasa kuhusu timu nyingine kusajili kwa gharama kubwa,” alisema Wenger na kuongeza:
“Siku zote lazima kuwe na timu moja, wakati mwingine hadi nne ambazo zinakuwa ni tajiri kuliko sisi nimejifunza kuishi katika mazingira hayo.
“Nafiriki jambo muhimu ni kupambana na mazingira yako kadiri unavyoweza, Manchester City ni matajiri zaidi yetu, hivyo ndivyo ilivyo kwa Chelsea na Manchester United lakini bado ninaamini tunaweza kupambana na kufanikiwa.”
Comments