Wawakilishi wataka bidhaa za Zanzibar ziondolewe vikwazo.

Related imageKamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi,  imeishauri Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kuweka mazingira bora zaidi kwa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani.
Lakini wameitaka kuziwekea vikwazo bidhaa zinazotoka nje ya nchi .

Wamesema kufanya hivyo kutasaidia kuimarisha viwanda vya ndani na kupata soko kubwa la bidhaa zinazozalishwa nchini.


Aidha wameitaka kuongeza ushirikiano pamoja na kuzitaka serikali zote mbili zikae pamoja ili kutatua baadhi ya changamoto za kisheria ili bidhaa zinazozalishwa Zanzibar ziweze kuingia katika soko la Tanzania Bara na lile la  Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa leo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo Yussuf Hassan Iddi  wakati akisoma hutuba kuhusu mswada wa sheria ya kuanzisha wakala wa maendeleo ya viwanda vidogo vidogo na vya kati Zanzibar pamoja na kuwezesha ushajiishaji na uendelezaji wa viwanda hivyo.

Kupitia Mwenyekiti huyo, kamati imeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa kuleta mswaada huo katika wakati muafaka nchi ikiwa katika mageuzi kutoka uchumi wa kutegemea kilimo kwenda uchumi wa viwanda.

Aidha alisema kuwa uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo na vya kati nchini utawawezesha wajasiriamali na wazalishaji wadogo wadogo kupiga hatua zaidi za uzalishaji pamoja na kupata masoko ya ndani na nje kupitia usimamizi wa wakala unaoanzishwa na sheria hiyo.

Alisema kwa kupitishwa mswaada wa sheria hiyo, Zanzibar itaweza kupiga hatua kubwa na kuzalisha ajira kwa vijana na kupunguza umasikini wa kipato kwa wananchi.

Alifahamisha kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi inategemea sekta ya viwanda kwa asilimia kubwa hivyo mswaada huu unaweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji na wajasiliamali wa nje na  wa ndani ili kuwekeza kwenye sekta ya viwanda .

Hata hivyo alisema kupita kwa mswaada huu kutaifanya Zanzibar kufungua milango ya fursa za kuinua uchumi na kupelekea pkuengezeka kwa pato la taifa (G.D.P).

Nae Waziri wa Biashara na Viwanda na Masoko Mheshimiwa Balozi AmIna Salum Ali alisema mswaada huu unaandika historia nyengine ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kujenga maisha ya wananchi ili  yawe mazuri katika kipato chao.

 Aidha alisemamswaada huo unaanzisha chombo ambacho ni wakala wa kusimamia maendeleo ya viwanda vidogo vidogo ,vidogo na vya kati baada ya serikali kuona changamoto mbali mbali zinazozikabili  viwanda hivyo na kuondoa mapungufu yanayojitokeza  na kuwawezesha wazalishaji kuwa na mazingira bora na kuzalishaji  bidhaa.

Nao Wajumbe wa Baraza hilo walisema  mswaada huo utasaidia vijana wengi kupata ajira lakini pia vijana hao waweke uaminifu katika uendeshaji wa  kazi zao  ili kuimarisha  viwanda hivyo.

Hata hivyo walisema nia ya serikali ni nzuri lakini  lazima ziondolewe changamoto mbali mbali zinazowakabili ikiwemo mikopo ukosefu wa mikopo rafiki kwa  wafanyabiashara kutokana na  kiwango kikubwa cha riba na soko la uhakika la kuuzia bidhaa hizo pamoja na suala zima la kusimamia ubora wa bidhaa hizo .

chanazo:zanzibar24.

Comments