Mkutano Mkuu wa CCM umemalizika mjini Dodoma, huku viongozi wastaafu wakipamba jukwaa kwa kueleza ya moyoni na wengine kutoa ushauri kwa viongozi wapya wa chama ambacho sasa kitakuwa na idadi ndogo ya wajumbe wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) na wale wa Kamati Kuu (CC).
CCM ilipanga kufanya mkutano huo wa kawaida kwa mujibu wa katiba ya chama hicho kwa msiku mbili (Desemba 18-19), lakini mkutano huo uliowachagua mwenyekiti, makamu wenyeviti wawili na wajumbe wa Nec, ulipambwa na matukio kadhaa hasa hotuba za viongozi wastaafu wakiwamo Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume, mawaziri wakuu wastaafu, Dk Salim Ahmed Salim, Mizengo Pinda na Katibu Mkuu wa CCM mstaafu Yusuf Makamba.
Makamba ambaye amekuwa Katibu Mkuu wa chama kuanzia 2006 hadi 2011 alitoa salamu zake kwa wajumbe wa mkutano mkuu kwa kuusifu msimamo wa mwenyekiti wa chama Taifa, Rais John Magufuli kwa kusimamia yale anayoaamini bila woga ikiwamo kukataa ushauri ambao anaona hauna tija.
Kiongozi huyo ambaye ni hodari katika uzungumzaji wa kutumia vitabu vya dini aliamsha shamrashamra alipopanda jukwaani na kummwagia sifa Rais Magufuli. “Tunakufahamu kuwa wewe una uwezo mkubwa wa kazi ya urais na ndiyo maana Kamati Kuu ilipokutana ikakupendekeza. Wewe ndiye unastahili kuwa mwenyekiti wa CCM kwa kuwa moja ya matatizo tunayoyapata ndani ya CCM ni watu kutosema ukweli, wanageuza matatizo, fitina ndiyo ukweli,” anasema Makamba.
Akionyesha kama vile alikuwa na jambo moyoni kiongozi huyo ambaye anapozungumza haachi kumchekesha anayemsikiliza alimtumia neno Rais Magufuli kuwa “Kuna siku nilikutumia meseji ukaniambia ushauri mbovu huutaki, hivyo ndivyo inavyotakiwa mimi sikukasirika.
Lakini, Makamba aliamua kuwachekesha wajumbe wa mkutano huo kwa kusema, “Mwenye uwezo wa kusema wapumbavu ni Mkapa. Mzee Mwinyi hawezi kwa kuwa ni muungwano, Kikwete hawezi kwa kuwa ni muungwana mimi siwezi kwa kuwa ni muungwana.”
Makamba ambaye anajulikana kwa baadhi ya watu kwamba ni ‘mtabiri wa kusadikika’ anasema, “wakati tunakuja kwenye mkutano huu, mama mmoja akamtumia meseji mama January akimuuliza ‘yule mtabiri wa kusadikika safari hii yupo’. Mama January akanionyesha ile meseji nikamuuliza mtabiri wa kusadikika ni nani akijibu si wewe. Nikamjibu mwambie nipo.”
“Kwenye ukumbi huu nilitabiri hapa kwamba Kikwete aliwabatiza kwa majii huyu anayekuja atawabatiza kwa moto. Na sasa yametimia kwenye uchaguzi wa marudio wa kata 43, CCM imechukua kata 42 na upinzani kata moja. Huo ni ubatizo wa moto. Na mwaka 2020 watapita kapa.”
Utaratibu wa viongozi hao wastaafu kusalimia wajumbe ulitekelezwa na aliyekuwa mwenyekiti wa muda kwenye mkutano huo, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa ambaye alianza kumwita waziri mkuu mstaafu kuanzia awamu ya kwanza hadi ya pili, Cleopa Msuya. “Kuna mtu hajmamsikia siku nyingi wacha nimuite aje kuwasalimia. Namwita Cleopa David Msuya aje kuwasalimia.” Hata hivyo, shauku ya kumtaka Msuya ayoe neno kwa wajumbe ilikatika pale alipoeleza kwamba hajisikii vuzuri.
Hiyo ilikuwa ni baada ya Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuhutubia wajumbe kwa kusema alitambua fika kuwa Rais Magufuli nduye mtu anayestahili kwenye nafasi hiyo licha ya kupata maswali kutoka kwa watu walionyesha wasiwasi. “Nilimtetea Magufuli watu walihoji hajawahi kuwa hata mjumbe wa shina iweje ghafla aje kuwa mwenyekiti wa chama. Nikawaambia ataweza kwani hahitaji shule,” anasema Kikwete.
Anasema katika kipindi cha miaka miwili, Rais Magufuli amefanya mambo makubwa yanayoleta matumaini na ameonyesha ujasiri wa hali ya juu. “Urais na uenyekiti hauna kwenda kusoma, unasomea humohumo ndani ukishapa ile dhamana bora akili yako iwe nzuri. Ikiwa mbovu ndiyo inaweza kuleta shida, lakini huyu wa kwetu yupo vizuri tena kaongezea na PhD, tuna kila sababu ya kushukuru tumepata kiongozi mzuri,” anasema Kikwete.
“Mpaka sasa ‘big up’ mtani wangu. Kazi hii ngumu sana, sababu mimi nimeifanya. Katika kazi ngumu duniani hii ndiyo kiboko. Uzuri na ubaya wa kazi hii ina upweke mkubwa.” Anasema Kikwete ambaye anaongeza kuwa kuhusu malalamiko ya hali ngumu ya maisha “Kuweni na Subira, viongozi wetu makini wanatambua matatizo yanayoakabili wananchi na nina aamini wanayatafutia ufumbuzi.”
Mwenyekiti Mkapa pia alimuomba Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume asalimie wajumbe ambaye licha ya kusema kwamba hakuwa ametarajia kupewa nafasi ya kuzungumza lakini mazungumzoa yake yalionekana kuwachangamsha wajumbe.
Karume aliyewahi kuitwa ‘simba mtoto’ kwakuwa ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume (marehemu) anasema utaratibu wa CCM kwenye mkutano kama huo, mwenyekiti mar azote amekuwa Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
“Utaratibu wetu kwa vikao kama hivi Mzee Mwinyi ndiye huwa mwenyekiti, lakini safari hii amesema hapa mimi nimekuja kuangalia tu. Nakupongeza kwa hilo Mzee Mwinyi. Pia, Mzee Mwinyi amekuwa akisema kila zama na kitabu chake. Kila utawala na wakati wake.”
Karume ambaye kwenye hotuba yake alikumbushia maisha yake ya ujana akiwa mbunge na Philip Mangula ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, walikuwa na nywele ndefu tofauti na ilivyo sasa kwa kuwa zama zao zimekwisha pita na sasa ni zamu ya vijana.
Anasema uwepo wa idadi kubwa ya viongozi wapya serikalini umetoa taswira ya kuimarika kwa chama ambapo aliwataka wajumbe ambao hawakuchaguliwa kwenye nafasi walizoomba kuendelea kufanya shughuli za chama.
Mwenyekiti Mkapa aliyesifika kwa uwazi na ukweli na wakati akigombea nafasi ya urais alitambulishwa kuwa ni ‘Mr Clean’ , alimwita jukwaani waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda kwa kumtaja kwa jina la utani, “sasa namwita mtoto wa mkulima.”
Pinda naye kama Karume, lakini yeye haikuwa tu kushitukizwa bali alijilinganisha kwa kutumia umri. “Mimi nilidhani maneno yaliyotolewa na wazee wangu yametosha. Sasa nimeitwa na mimi bwana mdogo. Siku chache zilizopita nilikuwa China na huko nilijifunza. Mambo mawili nilijifunza huko nadhani hata nilikueleza muheshimiwa Rais.
Anasema alimuuliza swali mmoja wa viongozi wa chama tawala cha China akitaka kufahamu idadi ya wanachama wao. “Alinijibu atanipa kitabu ambacho kitanisaidia kupata majibu. Alinipa vitabu viwili ‘volume one and two’. Nilipopitia kwa haraka haraka niligundua kuwa idadi kubwa ya wananchama si hoja unaweza kuwa na idadi ndogo ya wanachama ambao mwelekeo wao utaeleza sera nzuri za chama.
Pinda anasema hata wananchama wanaokuja hivi sasa kutoka upinzani ni kwamba wameona namna Rais Magufuli anavyofanya kazi. Na utendaji huo mzuri ndiyo umekuwa ukielezwa na kila anayerudi CCM.
Mkapa alipomsimamisha Dk Salim Ahmed Salim, yeye alizungumzia kwa kulinganisha na vyama vingine vya nje ya Tanzania, hasa chama cha ANC cha nchini Afrika Kusini kwama kwa kuwa kina umri mrefu kilikuwa kikitazamwa kama mfano wa kuigwa lakini kwa sasa kina hali mbaya kwa maana ya migogoro ya ndani.
Dk Salim ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Jumuiya ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa alisema chama pekee katika Afrika ambacho kimebaki kuwa mfano ni CCM, hivyo kuwataka viongozi waliochaguliwa kuendeleza hali hiyo
Anasema licha ya CCM kupitia katika hatua mbalimbali lakini imeendelea kuwa chama cha mfano katika kudumisha demokrasia na kukifanya kuwa chama cha mfano miongoni mwa vyama vya Ukombozi katika Bara la Afrika na duniani kwa ujumla.
Comments