WANANCHI
wa kata ya Iyumbu katika jimbo la Dodoma mjini wamempongeza na
kumshukuru Rais Dk.John Magufuli kwa kuwarejeshea ekari 129 ambazo
zilitengwa kwa ajili ya makaburi ya Viongozi wa Kitaifa.
Rais
Magufuli alifikia uamuzi huo baada ya kupokea maombi ya Mbunge wa Jimbo
la Dodoma Mjini Anthony Mavunde wakati wa ufunguzi wa nyumba 300 za
Shirika la Nyumba Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu.
Wakizungumza
kuhusu hatua hiyo, wananchi hao wamesema wamepokea kwa furaha kubwa
sana na kwamba dhamira ya Rais ya kuwajali wanyonge imetimia.
Mmoja
wa wananchi hao, George Makapi amesema urejeshaji huo utawawezesha
kuendeleza maeneo yao ambayo yalichukuliwa tangu mwaka 2006 kwa lengo la
kutumiwa kuzikia viongozi hao.
Katika
maombi yake, Mavunde alimuomba Rais Magufuli kulirejesha kwa wananchi
eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya makaburi ya Viongozi wa Kitaifa kwa
kuwa ni zaidi ya miaka 7 imepita bila wananchi kulipwa fidia yoyote na
kushindwa kuyatumia maeneo hayo kwa shughuli za kilimo na ufugaji kama
walivyokuwa wanafanya awali.
Kufuatia
ombi hilo, Rais Magufuli ameagiza ekari zote 129 zirejeshwe kwa
wananchi kwa kuwa serikali haina mpango wa kulitumia eneo hilo kwa sasa.
Aidha
Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa kuwa
na Mbunge mchapakazi na anayewajali wananchi wake na ambaye amekuwa
mstari wa mbele kutetea maslahi yao.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments