Unaweza kusema mwaka 2017 ulianza na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba na kumaliza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu.
Kwa maana nyingine alianza Mramba wa Tanesco, anamalizia Mchechu wa NHC aliyesimamishwa kazi juzi.
Kwa nyakati tofauti, kuanzia Januari Mosi mwaka huu, vigogo wa taasisi, idara na wakala za Serikali ama wamesimamishwa kazi au kuondolewa katika nyadhifa zao kutokana na tuhuma kadhaa jambo linalowalazimu kusubiri hatima yao kutoka kwa mamlaka zao za uteuzi.
Vigogo hao ni kutoka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), NHC, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Hayo pia yamewafika vigogo wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii na Bodi ya Sukari.
Uamuzi wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kumsimamisha kazi Mchechu huenda ukawa ndiyo wa mwisho iwapo ndani ya siku 13 zilizobaki kuhitimisha mwaka 2017 hakutakuwa na uamuzi wowote wa aina hiyo utakaochukuliwa.
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, vigogo kadhaa wameathiriwa na hali hiyo wakiwemo mawaziri ambao waliondolewa ndani ya muda mfupi tangu walipoteuliwa.
Katika mabadiliko aliyoyafanya Oktoba 7, Rais John Magufuli aliwaondoa mawaziri wanne waliokuwepo katika baraza la awali ambao ni Profesa Jumanne Maghembe, Gerson Lwenge, Annastazia Wambura na Ramo Makani. Pia, Nape Nnauye aliondolewa mwezi Machi.
Januari Mosi, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mramba akiwa mkoani Kagera na kumteua Dk Tito Mwinuka kukaimu nafasi hiyo. Uamuzi huo ambao haukueleza sababu, ulichukuliwa muda mfupi baada ya Rais kuwaweka kikaangoni vigogo waliotangaza kupandisha bei ya umeme, akisema hatua hiyo ni ushahidi kuwa bado kuna majipu na ataendelea kuyatumbua.
Mei 15, Rais alitangaza kuivunja Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), huku Mkurugenzi Mkuu wake Mhandisi Paskasi Muragili akielezwa atapangiwa kazi nyingine.
Katika kuivunja CDA, Rais Magufuli aliagiza wafanyakazi wote wa mamlaka hiyo wahamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na ofisi nyingine za Serikali kwa kadiri inayofaa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Juni 11, alitangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi.
Jula 6, Rais Magufuli alimteua Waziri Kindamba kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu Septemba 23, 2016.
Kutokana na uteuzi huo, aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Dk Kamugisha Kazaura ilielezwa atapangiwa kazi nyingine.
Julai 13, Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), iliwaachisha kazi maofisa wake waandamizi 12 waliokuwa wamesimamishwa kazi tangu Juni, 2016 ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.
Kupitia tangazo lake, bodi hiyo ilisema wameachishwa kazi baada ya kubainika kuhusika katika ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na utaratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, ununuzi wa ardhi na ajira.
Walioachishwa kazi ni Yacob Kidula (Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Mkurugenzi wa Fedha), Chiku Matessa (Mkurugenzi wa Udhibiti, Hadhara na Majanga), Pauline Mtunda (Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Hesabu za Ndani) na Crescentius Magori (Mkurugenzi wa Uendeshaji).
Wengine ni Amina Abdallah (Meneja Utawala), Abdallah Mseli (Meneja Uwekezaji), John Msemo (Meneja Miradi), Chedrick Komba (Meneja Kiongozi-Mkoa wa Temeke), John Ndazi (Meneja Miradi) na Ramadhani Nasibu (Meneja Mkuu Usalama).
Novemba 5, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliagiza kusimamishwa kazi Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma kadhaa, ikiwemo ya kugawa vitalu vya uwindaji kinyume cha sheria.
Mkurugenzi huyo pia anahusishwa na tuhuma za kuihujumu Serikali kwa kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari zinazochochea mgogoro katika Pori Tengefu la Loliondo.
Novemba 9, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alimuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Mathew Mtigumwe kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Henry Semwanza.
Kwa agizo hilo mkurugenzi huyo alitakiwa kurejea kwa mwajiri wake ambaye ni katibu mkuu wa wizara hiyo kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine. Semwanza alihudumu katika nafasi hiyo akiwa mkurugenzi tangu mwaka 2011.
Katika uamuzi unaoweza kuwa wa mwisho kwa mwaka huu, Lukuvi kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alieleza amechukua hatua ya kumsimamisha Mchechu kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu F. 35 (1) cha Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009.
Mbali na Mchechu, Lukuvi ameitaka bodi ya shirika hilo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Huduma za Mikoa na Utawala, Raymond Mndolwa.
chanzo:Mwananchi.
Comments