Tanzania yatahadharishwa kwa kuipinga Marekani kuhusu Jerusalem.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi na kidiplomasia wamesema kwamba huenda Tanzania ikakosa misaada ya kiuchumi kutoka nchini Marekani baada ya kupinga azimio la Marekani kuhusu Jerusalem.

Tanzania imeendelea kushikilia msimamo wake wa kuutambua Mji wa Tel Aviv kuwa Mji Mkuu wa Israel, huku ikipinga hatua ya Marekani kutambua Jerusalem kuwa Mji Mkuu wa nchi hiyo.

Katika mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) uliofayika Disemba 21 mwaka huu, Tanzania iliungana na nchi nyingine 127 kupinga uamuzi huo wa Marekani, huku wakiitaka isitishe kutambua Jerusalem kama Mji Mkuu wa Israel na waache mpango wao wa kutaka kuhamisha ubalozi kutoka Tel Aviv kwenda mji huo.

Kabla ya kura hizo, Marekani ilitangaza kuwa inafuatilia kwa karibu upigaji kura na kwamba ingesitisha misaada kwa nchi zote ambazo zitaenda kinyume na mpango wake.

Dr. Ahmed Mtengwa ambaye ni mtaalamu wa masuala ya diplomasia amesema kwamba, Tanzania inatakiwa kufanya maamuzi kutokana na seri zake za diplomasia ya uchumi.

Tanzania iungane na upande ambao utakuwa na manufaa kwake, kwa kuzingatia sera za diplomasia ya uchumi, alisema Dr. Mtengwa.

Waziri wa Mambo Nje wa Tanzania, Balozi Mahiga amesema kwamba, ubalozi wa Tanzania utaendelea kubakia Tel Aviv, na si kweli kwamba utahama au wamekwisha kuuhamisha kama ambavyo inadaiwa.

Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, Mchungaji Peter Msigwa amesema, hakukuwa na haja ya Tanzania kupiga kura, kwa sababu tayari ilikuwa imeshatangaza msimamo wake tangu awali.

Tanzania ilifungua ubalozi wake mjini Tel Aviv hivi karibuni, ambapo Israel inatarajia kufungua ubalozi wake nchini, mwakani. Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikihudumiwa na ubalozi wa Israel uliopo jijini Nairobi.

Tanzania ilianzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel mwaka 1963, lakini ulivunjika mwaka 1973 kufuatia vita ya Yom Kippur  iliyohusisha Israel, Misri na Syria.

chanzo: zanzibar24.

Comments