Rais
wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi amefanya ziara ya
kikazi ya siku moja hapa nchini ambapo amekutana na kufanya mazungumzo
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
Mjini Dodoma.
Mhe.
Filipe Jacinto Nyusi amepokelewa katika uwanja wa ndege wa Dodoma na
mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Makamu wa Rais Mhe.
Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na
kisha viongozi hao wamefanya mazungumzo rasmi na kusalimu wananchi
kupitia vyombo vya habari.
Mhe.
Rais Nyusi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumpokea na kufanya nae
mazungumzo na amesema ujio wake umelenga kuimarisha na kukuza zaidi
uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na kidugu kati ya nchi yake na
Tanzania.
“Mhe.
Rais Magufuli japo kuwa nimetoa taarifa ya muda mfupi kuwa nakuja
kuonana nawe, umenikaribisha umenipokea na tumezungumza mambo yenye
manufaa kwa nchi zetu, nakushukuru sana” amesema Mhe. Rais Nyusi.
Amebainisha
kuwa yeye na Rais Magufuli wamezungumzia namna Tanzania na Msumbiji
zitakavyobadilishana uzoefu kuhusu ugunduzi mkubwa wa gesi na mafuta
uliofanikiwa katika nchi hizi, masuala ya ulinzi na usalama na
uimarishaji wa miundombinu ya usafiri.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Nyusi kwa kuja
Mjini Dodoma na kwa kudumisha uhusiano na ushirikiano wa kidugu na
kihistoria uliojengwa na waasisi wa mataifa haya Hayati Baba wa Taifa
Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Machel wa Msumbiji.
Mhe.
Rais Magufuli amesema katika mazungumzo hayo pia wamekubaliana Tume ya
pamoja ya ushirikiano ya Tanzania na Msumbiji zikutane haraka ili
kuimarisha maeneo yote ya ushirikiano kwa manufaa ya nchi hizo.
“Nafurahi
kuwa Mhe. Rais Nyusi pia amesema Msumbiji itatoa kibali kwa Shirika la
Ndege la Tanzania (ATCL) kufanya safari za moja kwa moja kati ya
Tanzania na Msumbiji haraka iwezekanavyo, ili kurahisisha usafiri kati
yetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Nyusi ameondoka nchini jana jioni na kurejea nchini Msumbiji.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
chanzo:Mpekuziblog.
Comments