
Aidha, Karia alisema pamoja na mkakati huo ambao ni agizo la
Shirikisho la Soka duniani (Fifa), TFF haitakubali ubabaishaji
unaofanywa na klabu za Ligi Kuu kuhusu agizo la kuwa na timu za vijana
za madaraja tofauti.
Karia alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa TFF na wahariri wa
vyombo vya habari nchini uliofanyika katika Hoteli ya Sea Scape jijini
Dar es Salaam kwa lengo la kueleza walichokifanya kwa kipindi cha miezi
minne tangu walivyoingia madarakani na mikakati yao ya mbeleni.
Hata hivyo, rais huyo wa TFF alilazimika kutoa ufafanuzi huo wakati
alipoulizwa kuhusu maendeleo ya timu ya vijana inayoandaliwa kwa ajili
ya michuano ya Caf ya U-17 inayotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2019.
“Fifa haitaki ubabaishaji, hata sisi (TFF), imetuambia haitatueleza
ni lini inakuja kufanya ukaguzi wa mahesabu yetu, itakuja kwa
kushtukiza, hivyo kuna uwezekano ipo siku klabu zetu zikazuiwa kushiriki
michuano ya kimataifa kama hazitazingatia kuwa na viwanja vyao vya
mazoezi na mechi,” alisema na kuongeza.
“Pia kuanzia sasa na sisi hatutakubali ubabaishaji kwa klabu ambazo
zinaokoteza timu za vijana, tunataka kila klabu iwe na timu za madaraja
tofauti ya timu za vijana, vinginevyo kuanzia msimu ujao hatutaziruhusu
kushiriki Ligi Kuu.”
Agizo hilo la viwanja ni msumari wa moto zaidi kwa klabu kongwe Simba
na Yanga zinazodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya
SportPesa, ambazo mara nyingi zimekuwa zikiiwakilisha Tanzania Bara
kwenye michuno ya kimataifa, huku zikiwa hazina hata uwanja wa mazoezi.
Azam ambayo nayo imekuwa ikiiwakilisha nchi kwenye michuano ya
kimataifa, licha ya uchanga wake Ligi Kuu Bara ukilinganisha na wakongwe
hao, yenyewe imekidhi vigezo hivyo kutokana na kuwa na viwanja vyake
ambavyo vinakubalika na Fifa.
Akizungumzia baadhi ya mambo ambayo wameyafanikisha kwa maendeleo ya
soka la Tanzania, Karia alisema ni pamoja na kutatua tatizo la ulipaji
kodi TRA pamoja na makato ya mifuko ya jamii lililokuwa likiikabili TFF.
Karia pia alisema kutokana na uwezo mdogo kifedha unaolikabili
shirikisho hilo, hawataweza kujenga shule za kulea vipaji, lakini
mkakati wao wa kukuza vipaji, wameanza kwa kutumia mashindano ya shule
za msingi na sekondari kupitia Wizara ya Tamisemi.
Kadhalika, Karia alitolea ufafanuzi kuhusu kituo cha michezo
kinachojengwa Tanga kwa kufafanua kuwa ujenzi huo ni kama ulivyo ule wa
Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
“Tutakaa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Paul Makonda), ili
kuangalia uwezekano wa kupata eneo kwa ajili ya kituo kingine kama hiki
cha Karume, lakini ujenzi huo hautakuwa Ilala ama Temeke,”
alisema.Aidha, Karia amefuta mashindano yoyote ya soka yaliyo nje ya
mfumo wa TFF isipokuwa tu kwa kibali maalum.
Alisema mashindano ya soka yasiyo rasmi kama yale yanayoandaliwa na
wanasiasa majimboni na hata na baadhi ya taasisi na wadau, sasa yanapswa
kuandaliwa kwa mujibu wa kanuni za TFF kupitia wawakilishi wao eneo
husika.
Karia alisema wakati umefika sasa wabunge na wanasiasa kwa ujumla
kutoa fedha kuzidhamini timu za majimboni mwao badala ya kuanzisha
mashindano ya ng’ombe na mbuzi.
Comments