
Katika salamu hizo za rambirambi Dk. Shein alimueleza Waziri Dk.
Hussen Mwinyi kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa hiyo ya
vifo vya wanajeshi wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania vilivyotokea
tarehe 7 Disemba, 2017 katika Jamhuri ya Kongo.
Kuufuatia tukio hilo Rais wa Zanzibar alieleza kwua yeye binafsi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote wa Zanzibar
wanawakumbuka wanajeshi hao kwa ujasiri na uzalendo wao katika
kuhakikisha amani inapatikana katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na
maeneo yote ya Maziwa Makuu.
Aidha salamu hizo za rambirambi Dk. Shein alizitoa kwa Dk. Hussein
Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, familia za marehemu, ndugu, jamaa na
marafiki pamoja na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kutokana na msiba huo.
Salamu hizo zilimuomba MwenyeziMungu awape malazi mema mashujaa hao
pamoja na kuwaombea wanajeshi waliojeruhiwa wapate nafuu ya haraka na
kurejea katika hali zao za kawaida.
Sambamba na hayo, salamu hizo za rambirambi zilimuomba MwenyeziMungu
awape Watanzania wote moyo wa subira na uvumilivu katika kiipndi hiki
kigumu cha msiba huu.
Tukio hilo limetoa katika Kambi ndogo ya Semuliki iliyopo Kaskazini
Mashariki mwa Wilaya ya Beni katika Jimbo la Kivu baada ya kuvamiwa na
waaasi wa kundi la ADF katika eneo hilo la Mashariki mwa nchi hiyo ya
Kongo.
Tukio hilo limeelezwa kuwa ni baya zaidi kuwahi kutokea kutekelezwa
na waasi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa (UN) katika historia
ya miaka ya hivi karibuni.
Katika kipindi cha miezi sita tukio hili ni la pili kutokea baada ya
Oktoba mwaka huu wanajeshi wawili wa JWTZ waliokuwa katika kundi la
walinda amani kuripotiwa kuuwawa na wengine 18 kujeruhiwa.
Mbali na hao askari wengine wawili pia, waliripotiwa kuuawa mwezi Mei
2015 katika eneo la Kivu Mashariki mwa Kongo na mwengine wawili
hawakujulikana walipo baada ya kuvamiwa na waaasi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kulaani vikali shambulio hilo ambalo
halijawahi kutokea tokea JWTZ lianze kushiriki ulinzi wa amani nchini
DRC mwaka 2011.
chanzo: Zanzibar24.
Comments