KAMANDA
wa Polisi Kikosi cha Tazara, Patrick Byatao amesema wafanyakazi wasio
waaminifu wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara)
wanalisababishia hasara shirika hilo kutokana wizi wa mafuta katika
treni.
Akizungumza
katika hafla ya kuwapa zawadi wafanyakazi bora 10 wa mwaka 2017, Dar es
Salaam jana, Kamanda Byatao aliyataja maeneo korofi ambayo wizi huo
hufanyika kuwa ni pamoja na stesheni ya Mlimba (Kilombero), Makambako
(Njombe), Kongaga (Mbarali), Mpemba (Songwe) na Tunduma.
Alisema
watumishi hao hususani madereva wamekuwa wakishirikiana na wananchi
kuiba mafuta na ndiyo maana shirika hilo haliendelei. Kamanda Byatao
alisema kuwa Oktoba 7, mwaka huu, walifanikiwa kumkamata dereva wa
treni, Kagwa Ruoga na Mathew Mkula ambao walikuwa wakiendesha treni
lililobeba shaba kutoka Zambia kwenda Dar es Salaam na kwamba huku treni
hilo likiwa linatembea waliingiza watu watano na kuanza kuchukua mafuta
ya dizeli.
Aliwataka
wananchi kutoshiriki katika matukio hayo ya uhalifu na kwamba watumishi
hao watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuhujumu uchumi.
Aidha,
aliwataka askari hao kufanya kazi kwa uadilifu na kuwa wadadisi ili
kugundua matukio mbalimbali ambayo yanaweza kuhatarisha maisha.
Mmoja
wa askari waliopata zawadi, Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Tazara,
Insepkta Halid Kingazi alisema kuwa wataendelea kupambana na uhalifu ili
kuhakikisha wizi unaofanywa unaisha na shirika kubaki salama.
Kingazi
alisema kuwa waendesha mashitaka wanapaswa kuwapa ushirikiano kwa
kuhakikisha kesi wanazozipeleka mahakamani zinakwisha kwa wakati.
Kikosi
hicho kimetoa zawadi kwa askari wake walipo makao makuu Tazara, Kituo
cha Mlimba Kilombero na Iyunga Mbeya ambapo treni hiyo inapita.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments