Mwenyekiti
wa CCM mkoani Mwanza, Anthony Diallo amedai kukerwa na kitendo cha
maofisa wa Takukuru kusimamisha gari lake na kulipekua, wakati alipokuwa
kwenye harakati za kampeni wilayani Ukerewe.
Hali
hiyo, imekuja wakati uchaguzi wa viongozi wa CCM ukiwa umefikia ngazi
ya mkoa huku katika baadhi ya mikoa kukiwa na malalamiko mengi ya
rushwa.
Akizungumza wakati akiomba kura jana, Diallo alisema amesikitishwa na kutofurahishwa na kitendo cha maofisa hao.
“Kitendo
hiki (cha gari kupekuliwa), hakikuwa cha kiungwana,” alisema Diallo
ambaye anamiliki kampuni ya Sahara Media inayomiliki kituo cha
televisheni na redio.
“Hata mimi najua rushwa ni adui wa haki na nimeahidi kupambana na rushwa kwa ahadi na imani ya mwana CCM.”
Mbali
na kupekua gari la waziri huyo wa zamani, Takukuru iliwahoji baadhi ya
wagombea na wanachama mkoani Simiyu kwa tuhuma za rushwa.
Wakati
mkuu wa Takukuru mkoani Mwanza, Ernest Makale akithibitisha kupekuliwa
kwa gari la Diallo, mwenzake wa Simiyu, Adili Elinipenda amesema taasisi
yake inawashikilia viongozi na wanachama kadhaa kwa mahojiano.
Kuhusu
gari la Diallo kupekuliwa, Makale alisema tukio hilo lilitokea wilayani
Ukerewe baada ya maofisa wa Takukuru kupata taarifa kuwa kiongozi huyo
aliyekuwa wilayani humo kufanya kampeni alikuwa akijihusisha na vitendo
vya rushwa.
“Hata
hivyo, baada ya kulisimamisha gari yake na kufanya upekuzi, hatukukuta
ushahidi wowote na kumuachia kuendelea na kampeni zake,” alisema Makale.
Diallo
aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu
ya Nne, ni miongoni mwa wagombea waliopitishwa na Halmashauri Kuu
kutetea nafasi yake.
Katika
tukio la Simiyu, Elinipenda alisema Takukuru inaendelea kuwahoji baadhi
ya viongozi na wanachama wa CCM lakini hakuwa tayari kuwataja.
“Nitatoa taarifa na kutaja majina ya tunaowahoji baada ya zoezi la kuwahoji kukamilika,” alisema Elinipenda.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments