Kauli hiyo waliitoa jana kwa nyakati tofauti walipozungumza na Mwananchi baada ya mmoja wa wafungwa hao, Gerald Deus (30) mkazi wa Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita aliyetoka gerezani Desemba 9 kwa msamaha wa Rais John Magufuli kujikuta akirudi jela kwa miaka 15.
Mfungwa huyo alihukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya Mwanzo Bukombe baada ya kukiri kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu.
Deus alihukumiwa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Damas Gakwaya baada ya kukiri kosa la kupora Sh300,000 kutoka kwa Dina Mwende, mfanyabiashara wa soda za jumla wilayani Bukombe.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Bisimba alisema kuwaachia huru ni jambo jema, lakini kinachopaswa kufanywa na Serikali ni kuwasaidia jinsi ya kuishi katika jamii.
“Mtu anatoka gerezani hana nini wala nini na wakati mwingine hawajaandaliwa kuja kuishi kwenye jamii, mfano kuna mfungwa alifungwa akiwa na miaka 12 ametoka na miaka zaidi ya 50, sasa huyu anakujaje kuishi kwenye jamii,” alihoji Dk Bisimba.
Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), James Seka alisema: “Hadi mtu anaachiwa anakuwa kakidhi vigezo, lakini kuna umuhimu wa jamii ikaandaliwa ili kuja kuishi nao kwani baadhi wanarudi huku mtazamo wao kwa jamii haujabadilika.”
Mwenyekiti wa Parole, Agustine Mrema alisema Rais Magufuli hakurupuki kumwachia mtu, bali anakuwa amepata taarifa kutoka kwa wakuu wa magereza na vyombo vingine hasa kwa mfungwa kuwa amekiri kosa lake na kuahidi kutorudia.
“Wakati mwingine ni tabia, mtu anajutia kosa na kuahidi kutorudia ila sisi binadamu baadhi ni vigeugeu kwenda kinyume na ndicho kinachotokea kwa baadhi yao,” alisema Mrema ambaye pia ni mwenyekiti wa TLP.
Msemaji wa Magereza nchini, Lucas Mboje alisema wamekuwa wakitoa ushauri mbalimbali kwa wafugwa ili kuachana na tabia zinazoweza kuwaweka matatani kwa kuwa hiyo ni sehemu ya wajibu wao.
chanzo:Mwananchi.
Comments