Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei amesema hatoongeza muda wa
kuiongoza taasisi hiyo baada ya mkataba wake kukamilika Mei, 2019.
Mkurugenzi
huyo atakayekuwa ameiongoza CRDB kwa miaka 21 atakapostaafu, amesema
uamuzi huo anaufanya kupisha damu mpya kuendeleza mafanikio ya benki
hiyo kubwa nchini.
“Si
vizuri kung’ang’ania madaraka. Tunao wakurugenzi tuliowaandaa kwa muda
mrefu ambao wanaweza kuendeleza nitakapoishia. Ninapisha damu changa
nami nitaendelea kuwa mwanahisa wa kawaida,” amesema Dk Kimei leo
Alhamisi Desemba 28,2017.
Kwa
utaratibu wa benki hiyo, mchakato wa kumpata mkurugenzi mtendaji
huchukua miezi 18 lakini Dk Kimei ameongeza mwezi mmoja na kuifanya 19
ili kuipa bodi ya wakurugenzi nafasi zaidi ya kukamilisha hatua hizo.
Amesema
ingawa upo mfumo mzuri wa kurithishana madaraka ndani ya benki hiyo,
lakini mwenyekiti na bodi wana uhuru wa kumchagua mtu mwenye sifa za
ziada kutoka nje na kushirikiana na familia ya benki kuendeleza
mafanikio.
“Katiba
yetu inataka Mtanzania ndiye aiongoze CRDB. Ninaiamini timu
niliyoshirikiana nayo tangu niingie hapa. Hata benki nyingine
zinazotafuta wakurugenzi watendaji, ningezishauri zije CRDB,” amesema.
Ndani
ya muda uliobaki kabla mkurugenzi mpya hajakaribishwa, Dk Kimei amesema
angependa kuona inapata faida kama ya mwaka 2015 ilipotengeneza Sh187
bilioni ikiongezeka kutoka Sh148 mwaka 2014.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments