Mama yake Azory aiangukia Serikali kumpata mwanaye.

Mama mzazi wa mwandishi wa Azory Gwanda, Eva Mpulumba, ameiomba Serikali kumtafuta na kumresha mwanaye akiwa hai.
Azory (42) ambaye ni mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) anayefanya kazi Kibiti na Rufiji, mkoa wa Pwani ametimiza siku 21 tangu atoweke kwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana.
Akizungumza na gazeti hili kwenye mahojiano maalumu nyumbani kwake katika Kijiji cha Msimba wilayani Kigoma juzi, Eva alisema tangu apokee taarifa hizo, amejawa hofu kuhusu usalama na uhai wa mwanaye.
“Sijakata tamaa lakini nina hofu. Sina amani tangu nipate taarifa za mwanangu kutoweka, sijui nifanye nini nina mawazo mengi tangu nitape taarifa hizi,” alisema Eva anayekadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 80 kwa kuwa na yeye haikumbuki
Akionyesha uso wenye hofu na mashaka, mzazi huyo alisema watoto wake walimficha kuhusu tukio hilo hadi alipoelezwa na baadhi ya majirani waliofika kumpa pole.
“Watoto wangu walinificha taarifa hizi hadi majirani waliponiambia, nililia sana siku hiyo kiasi cha kutoweza hata kula chakula,” alisema Eva huku akijifuta machozi
Aliwaomba waliomchukua na kuendelea kumshikilia Azory kumwachia au kumfikisha kwenye vyombo vya sheria iwapo ana makosa. “Sijui alichowafanyia kiasi cha kutenda haya, lakini nawasihi wanirudishie mwanangu,” alisihi mzazi huyo.
Alisema kwa hulka, Azory ambaye ni mtoto wake wa tatu kati ya sita kuzaliwa ni mtu asiye na makuu, mwenye upendo kwa kila mmoja, mtiifu na asiyependa kumkwaza yeyote, hivyo anashindwa kuelewa kosa alilowatendea waliomchukua na kumshikilia.
Dada mkubwa wa Azory, Sophia Gwanda alisema familia yao inakesha kwa kuomba ili ndugu yao apatikane akiwa hai. “Taarifa za kuchukuliwa na watu wasiojulikana zimetupa hofu kutokana na matukio ya watu kupotea na wengine maiti zao kuokotwa wakiwa wameuawa, tuna imani Azory yuko hai na salama ipo siku wanaomshikilia watamwachia huru,” alisema Sophia na kuongeza: “Matukio ya watu kupotea na wengine miili yao kuokotwa kwenye fukwe za bahari na mtoni, ndizo zinatutia hofu zaidi tunapoona ndugu yetu ametoweka karibia wiki tatu sasa,” alisema Sophia.
Majirani wazungumza
Jirani wa familia hiyo, Rehema Daniel alisema tukio hilo limeibua hofu kijijini hapo hasa kwa ndugu, jamaa, marafiki na majirani wanaomfahamu Azory.
“Ni heri wanaomshikilia wangejitokeza kusema alichowakosea ili ndugu na jamaa tujue namna ya kufanya hata kama itabidi kuwalipa kama wanamdai, iwapo wamemuua watupe maiti tumzike tujue moja kuliko kutuacha katika hali hii,” alisema Rehema.
Naye jirani mwingine, Twalib Ramadhani aliwataka wanaohusika na kupotea kwa Azory kutambua Mungu pekee ndiye muamuzi wa haki na atawalipa sawasawa na machungu wanayoitendea familia na jamii yake.
Mmoja wa watu waliosoma darasa moja na Azory katika Shule ya Msingi Msimba, Yosia Sarutwe alisema taarifa za kupotea kwa rafiki yake huyo kumewapa hofu na kuiomba Serikali na vyombo vya dola kuongeza kasi ya kumtafuta.
chanzo:Mwananchi.

Comments