Mahakama yaruhusu baa 12 kuendelea na biashara Unguja.

Mahakama ya Vileo Zanzibar  imeziruhusu baa zote 12 zinazofanya biashara ya Pombe Wilaya ya kati kuendelea na biashara  hiyo kutokana na kukidhi vigezo  na masharti ya kisheria yaliyowekwa  na serikali.

Akitoa ruhusa hiyo huko katika Mahakama ya Wilaya Chwaka  Mwenyekiti wa Mahakama hiyo Mohammed Subeit amesema Bodi ya ukaguzi imefanya ukaguzi katika baa zote zilizopo wilaya ya kati ikiwemo Chwaka, Uroa na Marumbi na imejiridhisha  na utendaji wa wenye mabaa.


Amesema  vigezo wanavyoviangalia katika ukaguzi wa baa nchini ni  mazingira  ya eneo la biashara, ukataji wa lessen na vibali kwa mmiliki wa biashara hiyo,kama eneo litakuwa na fujo au malalamiko ya wananchi  sheria ya vileo inaruhusu baa hiyo kufungiwa lakini kama  vitakuwa hakuna tatizo lolote  hakutakuwa na  pingamizi kwa  mmiliki kunyimwa  kibali cha kufanyia biashara.

Hata hivyo amesema  wakati mahakama inaendelea na zoezi la kupokea maombi kwa wamiliki wa baa Watendaji wa mahakama hiyo hawakupokea malalamiko  wala tuhuma zozote kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya kati  kama  baa hizo zinaleta usumbufu au  matatizo yoyote.

Aidha Subeit ametoa wito kwa wamiliki wa baa kufuata sheria zilizowekwa na mahakama ya vileo  na pindipo wataepuka kufuata maagizo waliyoambiwa  mahakama haita sita  kuzifungia baa au kuwapokonya  vibali vya biashara hiyo.

Jumla ya baa 21 zimeruhusiwa kuendelea kufanya biashara ya pombe kwa mwaka 2018 kutokana na kukidhi vigezo.

chanzo:Zanzibar24.

Comments