Atakayechafua mazingira kutinga kortini.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggery Mwanri akihutubia wananchiMKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amezindua rasmi sheria ndogondogo za uhifadhi rasilimali na utunzaji mazingira ya vijiji vyote vilivyoko katika halmashauri ya wilaya ya Igunga na Mamlaka ya mji huo na kuonya kuwa atakayekamatwa akiharibu na kuchafua mazingira atafi kishwa mahakamani.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Makomero na Mwabakima vilivyoko wilayani humo katika hafla ya uzinduzi wa sheria hizo, alisema mazingira ya wilaya hiyo sasa yatakuwa bora kwa kuwa vitendo vya uharibifu vitadhibitiwa.
Alisema kukithiri kwa vitendo vya ukataji miti ovyo, kuchoma moto, kuharibu vyanzo vya maji na kujisaidia ovyo kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa sheria zinazoweza kuwabana wahusika katika vijiji na mamlaka ya mji.
Mwanri alifafanua kwa kuwa sheria hizo zimependekezwa na wananchi wenyewe, hata zilipofika ofisini kwake hakusita, alizipitia na kusaini moja kwa moja, hivyo akawataka kuzitekeleza ipasavyo ili kujiletea maendeleo.
Aliwataka wenyeviti wa vijiji, watendaji na madiwani kuzisambaza na kuhamasisha wananchi wao kuzisoma na kuzielewa ili watambue hatua za kisheria zitakazowakabili punde watakapokwenda kinyume nazo.


Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Makomero, Zefania Kilo alimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuzindua sheria hizo na kwa kuanzia alisema atahakikisha kila kaya inakuwa na choo bora na kupanda miti isiyopungua mitano.
chanzo:Habarileo

Comments