Zanzibar kufanya zoezi jengine la kugawa vyandarua na kupiga dawa majumbani.

Vongozi wa Wilaya, Halmashauri na Shehia kwa kushirikiana na taasisi zilizomo ndani ya maeneo yao wanalojukumu kubwa la kuhakikisha wanaendeleza mafanikio  mazuri yaliyofikiwa katika kupambana na maradhi ya malaria nchini.
Akifungua mkutano wa siku moja wa uhamasishaji kazi za Malaria uliowashirikisha viongozi wa Wilaya na Halmashauri za Unguja katika ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe,
Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Abdalla alisema mtazamo wa Wizara hivi sasa ni kufikiria njia nzuri za kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kupiga vita Malaria.
Alisema Zanzibar hivi sasa imefanikiwa kuwa na maradhi ya Malaria chini ya asilimia moja kitu ambacho ni adimu sana kufikiwa katika nchi zinazokabiliwa na maradhi hayo duniani.
“Mafanikio haya yanatokana na ushirikiano wenu katika kusimamia kazi za upigaji dawa majumbani na kuwahimiza wananchi matumizi ya vyandarua vilivyotiwa dawa,” alikumbusha Mkurugenzi Kinga.
Aliwataka viongozi hao kuongeza juhudi katika kuwahamasisha wananchi matumizi sahihi ya vyandarua kwani utafiti unaonyesha kuwa wananchi waliopatiwa vyandarua na kuvitumia katika njia sahihi ni asilimia 57 na malengo ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ni kufikia asilimia 82.
Dkt. Fadhil aliwashauri viongozi wa Wilaya na Halmashari kujiandaa na zoezi jipya la ugawaji wa vyandarua na upigaji dawa majumbani katika maeneo maalum ambayo wagonjwa wa maradhi hayo bado wanaendelea kupatikana.
Akizungumzia matayarisho ya zoezi la upigaji dawa majumbani mwaka 2018, msimamizi mkuu wa zoezi hilo Nd. Abdalla Rashid alisema jumla ya shehia 102 zikiwemo 89 za Unguja na 13 za Pemba zitapigwa dawa  kuanzia tarehe 20 Januari na kumalizika tarehe 11 Februari.
Alizitaja Wilaya zitakazopatiwa huduma yakupigiwa dawa kwa Unguja ni Magaharibi ‘A’ shehia tano, Magharibi ‘B’ shehia 11, Wilaya ya Kati shehia 35, Kaskazini ‘B’ shehia 13, Kakazini ‘A’ shehia 11 na Wilaya ya Kusini shehia 14
Alisema wameweka lengo la kupiga dawa nyumba 63,567 na kuishauri jamii kuwapa  ushirikiano vijana wataoendesha zoezi hilo  watakapo pita katika  maeneo  yao.
Wakati huo huo afisa anaesimaimia ugawaji wa vyandarua kutoka kitengo cha Malaria Mwinyi Khamis aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa kunzia mwaka 2018 kazi za kugawa vyandarua itasimamiwa na Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar kwa kushirikiana na vituo vya afya vilivyomo ndani ya shehia husika.
Aliwaeleza viongozi walioshiriki mkutano wa uhamasisha wa kupiga vita maradhi hayo kitengo cha malaria kimefanya utafiti na kuona kunahaja ya kushirikiana na taasisi nyengine katika kazi hiyo ili kuleta ufanisi zaidi.
Aliwataka wakuu wa vituo vya afya kushirikiana na Bohari Kuu ya Dawa kwa kupeleka mahitaji yao ya vyandarau kwa mwezi na katika hatua ya mwanzo itawahusu watoto chini ya mwaka mmoja na mama wajawazito.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Abdalla akifungua mkutano wa uhamasishaji kazi za Malaria uliowashirikisha viongozi wa Wilaya na Halmashauri za Unguja katika kitengo cha Malaria Mwanakwerekwe Mjini Zanzibar.

Meneja wa Kitengo cha Malaria Zanzibar Dkt. AbdallaSuleiman akiwaeleza viongozi wa Wilaya na Halmashauri mafanikio yaliyopatikana katika kupiga vita Malaria Zanzibar katika ukumbi wa Kitengo hicho Mwanakwerekwe.

Washiriki wa mkutano wa uhamasishaji kazi za kupambana na Malaria uliofanyika Kitengo cha maradhi hayo Mwanakwerekwe wakiwasikiliza watoa mada.

Afisa wa Kitengo cha Malaria Nd. Mwinyi Khamis akieleza utekelezaji wa mpango wa kugawa vyandarua katika ngazi ya shehia kwa mwaka 2018 katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe Mjini Zanzibar.

Msimamiza mkuu wa kupiga dawa majumbani aNd. Abdalla Rashid akitoa maelezo ya zoezi la upigaji dawa majumbani litakaloanza mwezi Januari mwakani katika shehia 102 za Unguja na Pemba.
Picha na Ramadhani Ali.
chanzo:zanzibar24.

Comments