
Alisema, serikali hufika wakati hulifidia ZSTC kutokana na
kujiendesha kihasara, hasa kutokana na bei ilipo sasa ya shilingi 14,000
kwa kilo moja, ambao inambeba mkulima kwa kupata asilimia 80 ya bei
hiyo.
Mhe: Aboud alieleza hayo, kabla ya kulitembelea shamba la serikali
lililoko Makuwe wilaya ya Wete, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua
shughuli za uchumaji na uuzaji wa zao la karafuu, linaloendelea
kisiwani Pemba.
Alisema ZSTC halifanyi biashara ya karafuu na wananchi, bali ni
kutekeleza agizo la serikali kuu, kuwahudumia wananchi na hasa wakulima
wa zao la karafuu, ili kutimiza malengo yao kwenye sekta hiyo.
Alisema tayari serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajali
wananchi wake, imshajidhatiti kuwa haitoshusha bei iliopo sasa, hataka
kama soko la dunia bei itashuka.
Hivyo, Waziri Aboud alisema, kutokana na ZSTC kujiendesha kihasara na
wakati mwengine kulazimika kuomba kuwezeshwa na serikali kuu, suala la
kupandisha bei mpya kwa sasa bado halijakuwa la kuwaweka kitako na
kulizungumza.
“Bei iliopo sasa ya zao la karafauu, ipo kwa ajili ya kuwaneemesha
zaidi wakulima wetu, na serikali imeshatamka mara kwa mara kuwa, bei
hiyo haitoshushwa, maana vyenginevyo, ni kuwaumiza wakulima
wetu”,alisema.
Katika hatua nyengine Waziri Aboud, aliitaka Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi kupeleka mpango kazi wa kuliimarisha shamba
hilo la Makuwe, ili liimarike zaidi.
Alisema shamba hilo ambalo ni tegemeo, kwa sasa linaonekana kuanza
kuchakaa kwa miti yake ya matunda na biashara, hivyo lazima uongozi wa
Wizara, ukae na wataalamu wake, ili wawe na andiko la kuliimraisha.
“Sasa inaoenekana miti kama mikarafuu imeshakuwa mikongwe, sasa hebu
tuleteeni mpango maalum wa kitaalamu, mutuombe ili kuliimarisha, maana
hii ndio hazina yetu”,alisema.
Katika hatua nyengine Waziri huyo kutoka Afisi ya Makamu wa Pili wa
rais, Mhe: Mohamed Aboud Mohamed, amewataka wale waliokodi mashamba ya
mikarafuu ya serikali, kufanya hima kurejesha fedha hizo.
Alisema kama kunachangamoto iliojitokeza baada ya zoezi la ukodishaji
kukamilika, wafike kwa wahusika ambao ni Wizara ya Kilimo, ili kufanya
mazungumzo ambayo yatasababisha kuondoa mivutano.
Mapema Mkuu wa Idara ya Misitu kisiwani Pemba, Said Juma Ali,
alimueleza waziri huyo, kuwa shamba hilo lenye hekta 79.7 linaundwa na
ploti 10, ambapo ndani yake mna mashamba sita yaliokwisha kodiwa kwa
thamani ya shilingi milioni 294.8.
Alisema kati ya fedha hizo, zilizokwisha lipwa na waliokodi ni
shilingi milioni 154, ambapo shamba hilo linaiingiza mapato makubwa
serikali, maana misimu iliopita ilianza na shilingi milioni 80, na sasa
kufikia shilingi milioni 294.8.
Mmoja kati ya wananchi waliokodi mashamba ya serikali, Jecha Mohamed
Faki, aliomba serikali kumuongezea muda wa kurejesha fedha alizotakiwa
kulipa, kutokana na msimu kuingiliwa na mvua.
Alisema, alikodi mashamba sita ya serikali kwa thamani ya zaidi ya
shilingi milioni 217, na tayari wastani wa shilingi milioni 120,
amesharejesha, ingawa ujio wa mvua zimesitisha uwanikaji na uvunaji.
Mapema Mdhamini wa ZSTC Pemba, Abdalla Ali Ussi, aliwataka wananchi
na wamiliki wa mashamha ya mikarafuu, kuendelea kufuata taratibu,
ikitokezea mchumaji ameangua mkarafuu.
Alisema ZSTC imeshakabidhi kiasi kikubwa cha fedha kwa Shirika la
Bima, kwa ajili ya kuwafanyia tathimini wananchi walioanguka wakati
waliokoa zao la taifa na kisha kulipwa.
“Hivi sasa, tunao tayari idadi ya watu 60 kwa Mkoa wa kaskazini
Pemba, pekee wakiwa wameshanguka kutoka juu ya mkarafuu, hivyo wakitokea
wengine waripoti kwa sheha, wapite Polisi na waende hospitali na
kukusanya taarifa zao”,alisema.
Wakati huo huo Waziri huyo na ujumbe wake, ulikagua kitalu cha miche
ya aina mbali mbali na wanakaya masikini wa shehia ya Mtambwe kaskazini,
waliojifufua upya, baada ya kitalu chao cha awali kutiwa moto.
Mratibu wa TASAF Pemba Mussa Said Kisenge, alisema kwa hatua za awali
wanakaya hao maskini, waliigawa bure miche kwa wananchi, ingawa kwa
mvuno wanatarajia kupanga namna ya kuwauzia ili nao kurejesha gharama
zao.
chanzo: zanzibar24.
Comments