Wasichana waathiriwa zaidi na maambukizi mapya ya VVU.

Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) imesema kundi linaloathirika na maambukizi mapya ya VVU ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, ambao ni sawa na asilimia 40 ya watu wanaopata maambukizi mapya kwa mwaka.
Tacaids imesema kati yao, asilimia 80 ni wasichana na asilimia 20 ni wavulana, hivyo kufanya katika kila vijana 10 wenye maambukizi mapya ya VVU wanane kuwa wasichana na wawili wavulana.

Mkurugenzi mtendaji wa Tacaids, Leonard Maboko (pichani chini) alisema jana kuwa, hali ya maambukizi mapya kwa sasa ni takriban watu 55,000 kwa mwaka, huku asilimia 40 wakiwa ni vijana. “Lakini hali inayotisha kundi ambalo grafu yake inazidi kupanda ni vijana ambao huchukua asilimia 40 kwa kila idadi ya watu wanaoambukizwa kwa mwaka, kinachosikitisha ukichukua kundi la vijana asilimia 80 ni watoto wa kike,” alisema.
Akizungumza wakati wa kuzindua mkakati wa Taifa wa kondomu na wiki ya maonyesho na huduma kuelekea maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani Desemba Mosi, naibu waziri wa mifugo na uvuvi, Abdallah Ulega alisema ni wakati sasa wa kuwekeza katika matumizi ya kondomu kwa vijana wa rika hilo.
Ulega aliyemwakilisha waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema mkakati huo unakusudia kuongeza matumizi ya kondomu kwa wanawake na wanaume kutoka asilimia 34 kwa wanawake na asilimia 40.5 kwa wanaume kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 55 mwaka 2018. Alisema kiwango cha matumizi ya kondomu kama njia ya kuzuia magonjwa ya ngono kinatishia kufikia malengo ya muda mrefu ya nchi, ikiwa ni pamoja na ya dunia ya sifuri tatu ifikapo 2030.
Ulega alisema kuwa kondomu zina uwezo wa kumkinga mtumiaji kwa asilimia zaidi ya 80. Mkurugenzi wa kinga wa Wizara ya Afya, Neema Lusibamaila alisema utafiti wa viashiria vya Ukimwi na malaria wa mwaka 2011/2012 ulibaini kuwapo kwa matumizi duni ya kondomu nchini.
Alisema ripoti inasema asilimia 69 ya wanawake na asilimia 77 ya wanaume miongoni mwa Watanzania watu wazima wanafahamu matumizi ya kondomu yanachangia kupunguza uwezekano wa mtu kuambukizwa virusi vya Ukimwi. “Katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018, Serikali kupitia wizara yangu kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria inatarajia kununua kondomu za kiume 500 milioni ambazo zitasambazwa nchi nzima,” alisema Lusibamaila.     
chanzo:Mwananchi.

Comments