Ucheleweshaji wa upepelezi na ukosefu wa umakini katika ushahidi chanzo cha kushindwa kwa kesi nyingi

hukumuHakimu mfawidhi wa Mahakama Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Moh’d Ali Moh’d amesema tatizo la ucheleweshwaji wa upepelezi wa kesi na kutokuwa makini katika utoaji wa ushahidi mahakamani kwa jeshi la polisi mkoani humo inapelekea kesi nyingi kushindwa kutolewa hukumu kwa wakati  mahakamani.

Hakimu Moh’d ametoa kauli hiyo huko katika makao makuu ya polisi Tunguu wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya wiki mbili kwa maafisa na askari wa jeshi la polisi mkoani humo yenye lengo la kuwajengea uwezo ili waweze kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.


Amesema  kumekuwa na mrundikano wa kesi nyingi katika mahakama za wilaya na mkoa ambazo zinajumuisha makosa mbali mbali yakiwemo ya ubakaji, kutorosha, madawa ya kulevya, ulawiti na ajali za barabarani jambo ambalo linapelekea kurudhisha nyuma juhudi za mahakama katika kuwapatia wananchi haki zao.

Aidha amewataka askari wa jeshi hilo kuzitambua na kuzifanyia kazi sheria zinazohusiana na makosa mbali mbali yakiwemo makosa ya jinai ili kuona kwamba wanaleta mabadiliko makubwa ndani ya jeshi hilo.

Nae akizungumza kwa niaba ya kaimu kamishna  wa polisi zanzibar kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi ndugu Saleh Mohd Saleh amesema umefika wakati wa askari wa jeshi la polisi kuondokana na kufanya kazi zao kwa kubahatisha na badala yake kuzingatia maadili na ueledi wa kazi zao  ili kuona kwamba wanaondosha malalamiko kwa wanachi.

Kwa upande wa kamanda wa polisi mkoani humo ndugu Makarani Khamis Ahmeid amesema jeshi la polisi  limeamua kutoa  mafunzo kwa askari wake baada ya kuona lina mapungufu na changamoto mbali mbali za kiutendaji.

 Chanzo:zanzibar24.

Comments