
Onyo hilo lilitolewa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni mstaafu George
Mkuchika alipokuwa anajibu swali la nyongeza lililoelekezwa wizarani
kwake na Zitto Kabwe.
Katika kujenga hoja yake, Mbunge huyo wa Kigoma Mjini
(ACT-Wazalendo), alisema nchi za Hungaria na Urusi ambazo Tanzania
imefuata nyayo zake kujitoa kwenye mpango huo ni miongoni mwa nchi
ambazo zinatuhumiwa kwa kuendeshwa bila misingi ya kidemokrasia na
kidikteta hivyo ni aibu kwa Tanzania kuiga nchi hizo.
“Majukwaa haya ya kimataifa yanatengeneza ushawishi kwa sababu Mwenyekiti wa OGP ni Canada,” Zitto alisema,
na “juzi Rais (John Magufuli) alisema serikali imemwandikia barua
Waziri Mkuu wa Canada kuhusiana na suala la (kuzuiwa huko kwa ndege ya)
Bombardier.
“Serikali haioni kwamba iwapo Tanzania ingekuwa
imeendelea kuwa mwanachama wa OGP, ombi hili la Rais lingeshughulikiwa
kwa uzito zaidi?”
Zitto alisema Manispaa ya Kigoma Ujiji ni miongoni mwa miji 15 ambayo
inashiriki katika OGP kwa uhuru na haizingatiwi kwamba nchi ipo kwenye
OGP au laa.
“Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na ushiriki si tu
wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ambayo inafaidika sana, lakini pia na miji
mingine ambayo pia inataka kuingia kwenye OGP?” Zitto alihoji.
Katika majibu yake, Mkuchika alisema Tanzania ilipofanya uamuzi huo
haikuiiga nchi yoyote bali ilifanya hivyo kwa kupima vigezo kwa
kuzingatia ilivyoona inafaa kutokana na Tanzania ni taifa huru
linalojitawala, linalofanya uamuzi wake lenyewe bila kushurutishwa na
taifa lolote, liwe kubwa ama dogo duniani.
Aliongeza kuwa Tanzania na Canada ni wanachama wa Jumuiya ya Madola
na Tanzania ina ubalozi Canada,hivyo kuwapo au bila kuwapo OGP,
mawasiliano kati ya nchi hizo mbili hayawezi kuwa tatizo.
Mkuchika alisema andiko la OGP linasema nchi ikijitoa, washirika wake
wote waliomo ndani ya nchi husika nao uanachama wao na shughuli zao
zinakoma.
“Serikali inayotaarifa kwamba Manispaa ya Kigoma Ujiji
mpaka sasa inawasiliana na OGP, na OGP wamemwandikia Waziri wa Mambo ya
Nje kwamba wana nia ya kuendelea kushirikiana na Ujiji,” Mkuchika alisema na kufafanua zaidi:
“Nataka kutumia bunge kuionya Manispaa ya Ujiji, nchi
inayozingatia utawala haiwezi kufanya maamuzi baraza la madiwani
likasema ‘sisi ‘hatuta-comply’ (hatutayafuata), haitotokea.
“Nataka niionye Manispaa ya Kigoma, waache mara moja,
watekeleze maamuzi ya serikali na wakiendelea kufanya mawasiliano kama
wanavyofanya sasa, serikali itachukua hatua kali zaidi na hatua hizo
kwenye manispaa ni kuvunja baraza la madiwani na kuweka tume ya
manispaa.
“Nawaomba huko mlipo wa Kigoma na Zitto msiifikishe serikali huko.”
Katika swali la msingi, Zitto alihoji sababu za serikali kuamua kujiondoa kwenye mpango wa OGP.
Akijibu swali hilo, Mkuchika alisema OGP ulitokana na wazo la Rais wa
Marekani, Barack Obama kwa lengo la kuzifanya nchi mbalimbali duniani
kuwa wazi katika uendeshaji wa shughuli za serikali.
Alisema mpango huo ulizinduliwa kama taasisi isiyo ya kiserikali
Septemba 20, 2011 na Tanzania ilijiunga Septemba 21, 2011 baada ya
kukidhi vigezo vya kujiunga ambavyo ni pamoja na kuzingatia misingi ya
utawala bora.
Alisema mpango huo ni wa hiari na nchi inaweza kujiunga baada ya
kutimiza masharti na hata kujitoa bila kuwapo kwa kizuizi chochote.
Waziri huyo alisema kuwa hadi sasa, nchi wanachama wa OGP ni 70 na kati yao, 10 ni kutoka barani Afrika.
“Baada ya serikali kushiriki utekelezaji wa mpango kwa
zaidi ya miaka minne imeamua kujitoa.
Tanzania si nchi pekee iliyojiunga
na mpango huo kisha kujitoa. Nchi nyingine ni kama Hungary (Hungaria)
na Urusi ambazo zilijiunga na kujitoa baadaye,” alisema.
Mkuchika alisema serikali tangu kupata uhuru imekuwa na ushirikiano
wa kikanda na kimataifa katika kutekeleza falsafa ya uwazi na
uwajibikaji.
Alisema serikali imejiunga na kutekeleza mpango wa kikanda na
kimataifa kama vile mpango wa nchi za Kiafrika wa kujitathmini katika
nyanja za utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa (APRM).
“Ni maoni ya serikali kuwa shughuli zinazotekelezwa na
kupitia vyombo hivyo zinatosha kwa nchi kuendelea kujijengea misingi
imara ya uendeshaji wa shughuli za serikali kwa uwazi, kuongeza
uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa,” alisema na kueleza zaidi:
“Nilihakikishie bunge kuwa Tanzania kujitoa katika mpango
huo hakuna madhara yoyote.
Mipango inayotekelezwa ndani ya nchi kama
ilivyoelezwa inajitosheleza kuendeleza na kuimarisha misingi hiyo ya
uwazi na uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa.”
chanzo: zanzibar24.
Comments