Serikali ya Libya kufanya uchunguzi kuhusu biashara ya utumwa.

Serikali ya Libya kufanya uchunguzi kuhusu biashara ya utumwaSerikali ya Libya yenye makao yake mjini Tripoli na ambayo inatambuliwa na jamii ya kimataifa imetangaza kuwa, itafanya uchunguzi kuhusiana na taarifa za kuweko biashara ya utumwa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Al-Aref al-Khoga, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Libya amewaambia waandishi wa habari mjini Tripoli kwamba, kumetolewa agizo la kuundwa kamati ya uchunguzi ili kujua ukweli wa mambo kuhusiana na taarifa za kuuzwa kama bidhaa wahajiri wa Kiafrika suala ambalo limekumbwa na radiamali kali kila kona ya dunia kulaani biashara hiyo ya utumwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya amesema, kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuwafuatilia wahalifu na wanaojihusisha na biashara ya magendo ya binadamu na utumwa nchini humo na kisha kuwafikisha katika mkono wa sheria.
Wiki iliyopita, televisheni ya CNN ilirusha hewani mubashara mnada wa kuuza Waafrika huko nchini Libya ambapo kila mtu alikuwa akiuzwa kwa kwa dola zisizopungua 400 za Kimarekani. Wamiliki wa mashamba ndio waliokuwa wanunuzi wakuu wa "watumwa" hao katika mnada huo. 
Katika radiamali yake, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mnada huo wa kuwauza Waafrika kama watumwa nchini Libya ni uhalifu dhidi ya binadamu
Libya ilitumbukia kwenye machafuko tangu mwaka 2011 baada ya madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kuingia kijeshi huko Libya katika kampeni ya kumng'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi. 
Tangu mwaka huo hadi hivi sasa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika haijawahi kushuhudia usalama na utulivu hata mara moja.
chanzo:parstoday.

Comments