Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutafuta fedha na
kujenga barabara ya Mutukula – Minziro yenye urefu wa kilometa 6 ili
kurahisisha usafiri wa watu na mizigo.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 11 Novemba, 2017 katika Mji wa
Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda baada ya kupokea kero za
wananchi waliokusanyika jirani na geti la kuvuka mpaka huo ambao wamedai
kukosekana kwa barabara hiyo kunawalazimu kutumia barabara ya kuzunguka
Kyaka.
Pamoja
na kumtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kujenga barabara
hiyo Mhe. Rais Magufuli pia amewataka viongozi wa Mkoa wa Kagera
kufanyia kazi madai ya wananchi waliolalamikia kupata usumbufu katika
kizuizi cha Kyaka jirani na mto Kagera.
Hata
hivyo Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wananchi wa Mutukula kutambua kazi
ya ulinzi na usalama inayofanywa na vyombo vya dola na amewataka kutoa
ushirikiano kwa viongozi na Serikali katika kuhakikisha mpaka huo
unakuwa salama.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi hao kuongeza juhudi katika
shughuli za maendeleo zikiwemo kilimo na biashara na amerejea agizo lake
la kuutaka Mkoa wa Kagera kujenga soko la kimataifa katika maeneo ya
jirani na mpaka huo ili wananchi wapate mahali pa kuuzia bidhaa zao kwa
njia halali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mutukula
11 Novemba, 2017
chanzo:Mpekuziblog.
Comments