NEC yatoa onyo kwa vyama vya siasa.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani ameonya kuwa chama au mgombea atakayekiuka maadili ya uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika  Novemba 26 mwaka huu, atachukuliwa hatua kama ilivyoanishwa chini ya Kifungu cha 124A cha Sheria ya Uchaguzi Na.1 ya mwaka 1985.

Akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya Uchaguzi huo amevitaka vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinawaelemisha wafuasi wao kwani iwapo wafuasi wa vyama vya siasa watavunja maadili, chama husika pamoja na mgombea wake kitachukuliwa hatua za kinidhamu.


Miongoni mwa vitendo vinavyokiuka maadili ya uchaguzi ni pamoja na wagombea au wafuasi wa vyama hivyo kuchana mabango ya wagombea wengine, kutoa lugha chafu wakati wa mikutano ya kampeni pamoja na kupitisha muda wa kufanya mikutano ya kampeni.

Amezitaka kamati za maadili za kata na jimbo kuchukua hatua kali ndani ya masaa 48 pindi vitendo hivyo vikijitokeza na adhabu itakuwa ni kuomba radhi wananchi hadharani, kutotumia vyombo vya habari kwa muda fulani, onyo la maandishi kusimamishwa kufanya kampeni, mgombea kutangaza mbele ya vyombo vya habari kuwa yeye ni bingwa wa kuvunja maadili ya uchaguzi au kutozwa faini Sh 100,000.

Kailima pia amesema chama kitakachotaka kufanya mabadiliko ya ratiba ya mikutano ya kampeni, lazima kimfahamishe msimamizi wa uchaguzi wa kata na ombi hilo litajadiliwa na vyama vyote vinavyoshiriki kwenye uchaguzi.

Vitambulisho mbadala vitakavyotumika  kupigia kura kwa wale ambao wamepoteza kadi ya mpiga kura ni vitambulisho vya taifa, leseni ya udereva na hati ya kusafirisha hata kama vimeisha muda wake, mhusika anaruhusiwa kupiga kura.

Wakati huo huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26, 2017 katika kata 43 utagharimu kiasi cha Sh bilioni 2.5.
chanzo: zanzibar24.

Comments