
Akihutubu moja kwa moja kupitia runinga ya taifa, Bw Mugabe amesema anapanga kuongoza mkutano mkuu wa chama mwezi Desemba.
Maafisa wakuu wa chama hicho cha Zanu-PF walikuwa wameidhinisha hatua
ya kumvua uongozi wa chama hicho na kumpatia saa 24 ajiuzulu la sivyo
wamuondoe madarakani.
Jeshi lilichukua udhibiti wa serikali wiki iliyopita, huku mzozo
kuhusu nani atamrithi ukizidi kutokota. Bw Mugabe ameonekana kupoteza
udhibiti wa chama chake.
Mzozo wa sasa ulianza Bw Mugabe alipomfuta kazi makamu wake Emmerson
Mnangagwa wiki mbili zilizopita, hatua iliyolikera jeshi ambalo
lilitazama hatua hiyo kama jaribio la kumteua mke wake Grace kuwa makamu
wa rais na mwisho kuwa mrithi wake.
Mapema Jumapili, Bw Mnangagwa alitangazwa kuwa kiongozi mpya wa chama
cha Zanu-PF na mgombea wake wa urais uchaguzi mkuu wa 2018.
Katika mkutano huo pia, Grace Mugabe, 52, alifukuzwa kutoka kwa chama hicho pamoja na maafisa wengine wakuu.
“Mkutano mkuu wa chama (cha Zanu-PF) utafanyika wiki chache zijazo na
nitauongoza na kusimamia shughuli zake,” Rais Mugabe ameliambia taifa
kupitia runinga, akiwa ameandamana na majenerali kadha wakuu jeshini.
Amekiri uokosoaji dhidi yake kutoka kwa Zanu-PF, jeshi na umma, na kusisitiza kwamba ipo haja ya hali ya kawaida kurejea.
“Bila kujali faida au madhara ya jinsi (jeshi) walitekeleza
operesheni yao, mimi, kama amiri jeshi mkuu, nakiri kwamba kuna
matatizo,” amesema, akirejelea hatua ya jeshi ya kuchukua udhibiti wa
runinga ya taifa wiki iliyopita.
Hata hivyo, hakuzungumzia uwezekano wake kujiuzulu.
Raia wengi nchini Zimbabwe wameonekana kushangazwa na hotuba ya Bw Mugabe ambaye alitarajiwa na baadhi yao kujiuzulu.
chanzo: zanzibar24.
Comments